BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu barani  Afrika (CAF), limekataa ombi la timu ya Yanga juu ya kubadili siku na muda wa mchezo dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

 Katika taarifa ya CAF iliyofika TFF imesema mchezo huo utafanyika Jumanne Juni 28,  saa 10.00 jioni kama ulivyopangwa awali katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo mabingwa hao waliomba   mchezo huo ufanyike Juni 29, 2016 saa 1.30 usiku.

Kadhalika, kikao cha maandalizi katika mchezo huo kilichofanyika leo  kimeagiza uongozi wa Yanga kuwaelimisha mashabiki wao kukaa katika eneo la mazoea tofauti na mipango yao ya kutaka kukaa eneo lote la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 Mtanange huo utachezeshwa na Sikazwe akisaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia na Berhe O’Michael wa Eritrea atakayekuwa upande wa kushoto huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba. 

Kamishna wa mchezo huo atakuwa Celestin Ntangungira wa Rwanda. Pia mchezo huo utakuwa na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza.

Aidha mapema leo Uongozi wa Yanga ulitoa taarifa kuwa mchezo huo hautochezwa jumatano usiku kama walivyopanga, badala yake utachezwa jumanne jioni kutokana na tatizo la jenereta katika uwanja wa Taifa.

Post a Comment

 
Top