BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar

UONGOZI wa klabu ya Majimaji umekiri kufanya mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa zamani wa timu ya Simba, Emmanuel Gabriel kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake msimu ujao.

Gabriel ambaye aliwika na Wekundu wa Msimbazi mwanzoni mwa miaka ya 2000 atakuwa mchezaji mkongwe zaidi ndani ya 'Wanalizombe' ambaye ataongeza hamasa ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo kwa kushirikiana na wazoefu wengine kama Danny Mrwanda, Fredy Mbuna, Godfrey Taita, Lulanga Mapunda na Oddo Nombo .

Meneja wa timu hiyo Godfrey Mvula ameiambia BOIPLUS kuwa mazungumzo yanaenda vizuri na muda mfupi kutoka sasa wataweza kumtangaza mshambuliaji huyo kama mchezaji wao mpya.

"Ni kweli tumezungumza nae, tupo kwenye hatua nzuri na tunatarajia muda si mrefu atakuwa mchezaji wetu," alisema Mvula.

Aidha Mvula alisema "Msimu ujao tumepanga kufanya makubwa zaidi, tunaanda kikosi kabambe cha ushindani. Lakini pia tunahitaji nguvu kubwa kutoka kwa mashabiki wetu na wakazi wa mkoa wa Ruvuma kwakuwa hii ndiyo timu yao pekee." 

Mtandao huu ulimtafuta Gabriel ambaye alikiri kupigiwa simu na viongozi wa Majimaji ingawa alidai kuwa bado haijafika hatua ya kulizungumzia hilo.

"Wamenipigia simu kunieleza nia yao, na kwavile mimi nipo tayari na nina uwezo wa kurejea ligi kuu basi nawasubiri wao tukae mezani kuzungumza, kama tutaafikiana utaniona ligi kuu msimu ujao," alisema Gabriel aliyepachikwa jina la Batgoal kutokana na uwezo wake mkubwa kwenye kupachika mabao. 

Katika hatua nyingine Mvula alisema wapo katika mazungumzo ya kuongeza mkataba na kocha wao Kali Ongala ambao umemalizika mwishoni mwa msimu uliopita.

Post a Comment

 
Top