BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda kwa Msaada wa Mitandao
MPIRA wa miguu ni moja kati ya michezo inayofanya wachezaji wake kuwa matajiri wakubwa hadi kupelekea kuanza kumiliki magari na majumba ya kifahari. Hii ni kutokana na malipo ya mikataba, mishahara na posho kubwa wanazopokea nyota hao.

Tayari soka la Bongo limeshaanza kuonyesha njia baada ya nyota kadhaa wakiwemo Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Juma Luizio, Uhuru Selemani, Mrisho Ngassa, Hamis Mroki na wengineo kufanikiwa kuvuka boda na kwenda kusakata kabumbu nje ya nchi. Wiki iliyopita kwenye siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa, Ulimwengu alijizawadia gari ya kifahari aina ya Chrysler Crossfire yenye thamani ya Sh 50 Milioni.

Si rahisi kuwakaribia wachezaji wakubwa barani Ulaya, lakini hizi ni ishara za mafanikio kwa wanasoka wa Tanzania.
Hapa nakuletea orodha ya wanasoka wanaomiliki 'mikoko' mikali na yenye thamani kubwa.

1. CRISTIANO RONALDO

Ukipenda muite 'Kichaa Magari', mara zote amekuwa akiongoza orodha ya wanandika wanaoendesha magari yenye thamani ya juu. Kwenye eneo lake la kupaki magari straika huyo wa Real Madrid na timu ya Taifa ya Ureno ana magari kadhaa ya kifahari.Licha ya Ferrari 599 GTO, Lamborghin na Royal Royce alizopaki, Ronaldo anaburuza 'ndinga' aina ya Bugatti Veyron (pichani) yenye thamani ya Dola 1.7 milioni ambayo ni zaidi ya Sh 3.6 Bilioni.

2. RONALDINHO GAUCHO

Huyu ndiye Mfalme wa ladha za mpira, alijipatia utajiri mkubwa alipokuwa akiichezea Barcelona ya nchini Hispania kutokana na mafanikio aliyoyapata na wakatalunya hao.Gaucho ni mtu wa kula 'Bata', na moja ya starehe zake ni kuendesha magari makali. Naye alivunja benki na kutoa Dola 1.7 Milioni kununa Bugatti Veyron kama ya Ronaldo. 

3. SAMUEL ETO'O

Bugatti Veyron inabakia kuwa gari pendwa kwa wanasoka wanaopenda magari makali, na hii ndio sababu raia wa Cameroon Samuel Eto'o aliamua kuungana na Ronaldo pamoja na Gaucho kuinunua gari hiyo kwa thamani ile ile.Kwasasa Eto'o amestaafu kucheza soka la kiushindani pamoja na timu ya taifa huku akibaki kucheza kwenye ngazi ya klabu tena katika timu zinazoshiriki ligi 'laini'.

4. ZLATAN IBRAHIMOVIĆ

Huyu ni mmoja wa wachezaji ghali sana katika klabu ya PSG. Analipwa pesa nyingi kuanzia mshahara, posho na mikataba ya matangazo. Pesa hizi zimemwezesha kufanya mambo kadhaa makubwa lakini magari ya kifahari kwake ni kama ugonjwa sugu.Ibrahimović anaendesha gari aina ya Porsche Spyder yenye thamani ya Pauni 616,500 ambazo ni zaidi ya Sh 2 Bilioni.

5. FRANK LAMPARD

Frank Lampard anabakia kuwa mmoja wa viungo wanaolipwa pesa nyingi duniani. Nyota huyo anayeitumikia Manchester City anamiliki Ferrari Scaglietti 612 ambayo kama hauna Pauni 200,000 huwezi kuitoa dukani. Hiyo ni zaidi ya Sh 600 Milioni6. NEYMAR
Akiwa ni straika wa kibrazili anayelipwa pesa nyingi zaidi kwenye ligi kuu ya Hispania La Liga, Neymar ameshindwa kuficha udhaifu wake linapokuja suala la magari.Nyota huyo wa Barcelona hakuona shida kulipa Dola 246,000 (zaidi ya Sh 500 Milioni) ili akabidhiwe funguo za Audi R8 GT ambayo anatanua nayo kwenye viunga vya jiji la Barcelona.

7. MESUT ÖZIL

Washika bunduki Arsenal chini ya kocha Arsene Wenger wamekuwa wagumu sana kusajili wachezaji ghali na hata kulipa mishahara mikubwa kwao imekuwa utata. Lakini ukiwataja wachezaji wanaolipwa vizuri kwenye ligi kuu nchini Uingereza basi hutoacha kumjumuisha Mesut Ozil.Ozil aliyesajiliwa na Arsenal akitokea Real Madrid anaendesha gari kali aina ya Ferrari 480 ambayo aliinunua kwa kiasi cha Pauni 169,000 ambazo ni zaidi ya Sh 500 Milioni.

8. GARETH BALE
Anatajwa kuwa winga bora zaidi duniani kwa sasa. Na hii ni kutokana na mchango wake mkubwa kwenye mafanikio ya klabu yake Real Madrid pamoja na timu ya Taifa ya Wales ambayo hivi karibu amefanikiwa kuipeleka katika hatua ya 16 bora ya michuano ya Euro 2016.Bale anaendesha Audi R8 GT nyeupe yenye thamani ya Dola 246,000 ambazo ukizicheji kwa pesa ya Bongo  basi haipungui Sh 500 Milioni.

9. WYNE ROONEY

Nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza ambaye hana makuu lakini kwenye suala la usafiri uzalendo ulimshinda.Rooney alilipa Pauni 150,000 (zaidi ya Sh 500 Milioni) kununua Aston Martin ambayo ndio gari yake ghali kuliko zote.

10. LIONEL MESSI

Ndio, ni Lionel Messi katika nafasi ya 10 kwenye orodha hii. Messi si mtu wa mambo mengi lakini licha ya ubahili wake, bado anaendesha Audi R8 Spyder aliyoinunua kwa Pauni 102,385 ambayo ni zaidi ya Sh 300 Milioni.


Post a Comment

 
Top