BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Shinyanga
HUKUMU ya kesi ya shambulizi la kudhuru mwili anayodaiwa kufanyiwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Mwanahiba Richard dhidi ya kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto itatolewa keshokutwa Jumatano.

Mwanahiba alidai kushambuliwa na Mwinyi Februari 10, baada ya mazoezi ya timu hiyo ilipokuwa inajiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United, mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.

Kesi hiyo ambayo ipo katika Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga inaongozwa na Hakimu Mfawidhi, Rahim Mushi ambapo wahusika wa kesi hiyo Mwinyi na Mwanahiba wote walikuwepo.

Hii ilikuwa ni mara ya nne ambapo awali ilitajwa tu lakini leo ilisikilizwa na kupangiwa siku ya hukumu huku mtuhumiwa akipewa nafasi ya kujitetea wakati mlalamikaji naye alijieleza.

Mwinyi pia aliwakilishwa na mwanasheria wake Kaunda wakati Mwanahiba aliwakilishwa na mwanasheria wa serikali Upendo Shemkole.

Hata hivyo, baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili hakimu Mushi alitoa muongozo kuwa kesi hiyo itatolewa hukumu Jumatano.

Post a Comment

 
Top