BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

BEKI wa kulia wa timu ya Prisons, Salum Kimenya amewataka Simba wakamilishe taratibu zote ili aje jijini Dar es Salaam kumwaga wino na kuwatumikia Wekundu hao msimu ujao.

Kimenya anawindwa na Simba ili kuchukua nafasi ya Hassan Kessy aliyetimkia Yanga huku beki mwingine Emery Nimubona  ambaye angeweza kuziba pengo hilo akiwa amesharejea kwao Burundi baada ya kumalizana na wababe hao wa Msimbazi.

Kimenya ameiambia BOIPLUS kuwa mazungumzo yake na Simba yanaendelea vizuri ila wanasuasua katika kukamilisha baadhi ya vitu ili aweze kutia saini na kuvaa jezi nyekundu na nyeupe msimu ujao.

Kimenya kushoto akipambana na straika wa Simba, Mganda Hamis Kiiza


"Mimi ni mwajiriwa huku, siwezi kuja Dar kama hatujamalizana, kikubwa ni Simba kumalizia mahitaji yangu ninayoyataka halafu nije kusaini," alisema Kimenya.

Awali kulikuwa na taarifa za beki huyo kusaini fomu za awali za Wekundu hao lakini alikana juu hilo na kusema kilichopo ni mazungumzo baina yake na viongozi wa Simba ambayo bado hayajakamilika.

" Sikuwahi kusaini Simba ila bado tupo kwenye mazungumzo japokuwa hatujafikia makubaliano bado," alisisitiza Kimenya.

Simba ipo katika harakati za kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye miaka ya hivi karibuni huku watani wao wa jadi Yanga wakipeta.

Post a Comment

 
Top