BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar
KINDA Malik Jafari Kapolo (pichani) ambaye aliwahi kung'ara na kikosi cha pili cha wekundu wa Msimbazi , Simba ya jijini Dar es Salaam ameitwa kufanya majaribio katika kikosi cha Thanda Royal Zulu ya Afrika Kusini.

Kapolo ambaye wenzake wamempachika jina la kiungo wa Arsenal Ozil (Mesut) kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuuchezea mpira, alijiunga na Simba B msimu wa 2013/14 kabla Ashanti hawajamchukua na kucheza ligi kuu ya Vodacom hadi 2015 iliposhuka daraja.

Kabla Ashanti haijashuka daraja, kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 alipata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi huko visiwani Zanzibar akiwa na kikosi hicho kabla hajarejea Simba B ambayo ilivunjwa baadae mwaka jana.

Kapolo (kulia) akipambana na walinzi wa Tusker FC ya Kenya katika mchezo wa kombe la Mapinduzi mwaka jana. Picha kwa hisani ya BIN ZUBEIRY

Kapolo anayemudu vizuri winga zote mbili amefanyiwa mpango wa kwenda kujaribiwa Bondeni na winga wa Royal Eagles, Uhuru Selemani ambaye yupo nchini kwa mapumziko mafupi.

"Nipo likizo huku nikishughulikia safari ya huyu bwamdogo, Thanda wanahitaji mchezaji wa aina yake mwenye umri mdogo kwahiyo nina hakika atafuzu kwavile uwezo anao," alisema Uhuru ambaye amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi chake.

Tayari Kapolo anatajwa katika wachezaji wanaohitajika na Yanga kwa ajili ya kuunda kikosi cha pili imara cha timu hiyo (U20) ambacho kitakuwa chanzo cha wachezaji wa kurithi mikoba ya wakongwe wa wanajangwani hao.

Post a Comment

 
Top