BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
 ALIYEKUWA beki wa Simba, Emiry Nimubona raia wa Burundi aliikimbiza familia yake mapema akidai kuwa alishtukia dili la kutoongezewa mkataba ambapo sasa yupo kwao na ameachwa kwenye kikosi hicho rasmi.

Nimubona aliuomba uongozi wake umpatie nyumba ili aweze kuileta familia yake kwani nchini kwao kuna machafuko ya kisiasa hivyo alishindwa kucheza kwa kiwango cha juu kwani alidai kutumia muda mwingi kuiwaza familia yake.

Akizungumza na BOIPLUS, Nimubona alisema kuwa alishitukia mpango huo tangu Simba ilipotolewa kwenye michuano ya Kombe la FA baada ya kufungwa na Coastal Union ndipo alipoiondoa familia yake nchini.

''Unajua hata kabla ya kusaini Simba mke wangu hakupenda nije kucheza huko, mimi nilitaka kwani ndiyo kazi yangu hivyo ilimbidi tu aniruhusu ila nilipoona mambo yameanza kuharibika ndani ya Simba niliona ni vyema kuiondoa familia yangu ili isishuhudie yaliyokuwa yanaendelea.

''Hakuna kiongozi aliyejuwa kuwa familia yangu nimeirudisha nyumbani, nilifanya mambo yangu kimya kimya kwani nilijua mke wangu pengine angeathirika kisaikolojia akiona jinsi mambo yanavyokwenda wakati alinipa tahadhari,'' alisema Nimubona.

Beki huyo alisema kuwa anaamini hatakosa timu ya kuichezea ambapo anaangalia zaidi nchi za Rwanda na Kenya hata nyumbani kwao Burundi ingawa alidai ligi ya kwao haina masilahi mazuri.

Post a Comment

 
Top