BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
LICHA ya Taifa Stars kutocheza vizuri dhidi ya Misri lakini kocha wa Mapharao hao, Hecter Raul Cuper amekiri nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta ni mchezaji bora na anamtabiria kufika mbali zaidi.

Hecter aliyazungumza hayo katika kikao na waandishi wa Habari baada ya kumalizika kwa mchezo huo na kukiri kuwa Stars itakuja kuwa bora zaidi siku za usoni kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye vipaji ila uchanga katika michuano hii ndiyo kinachowaangusha.

Kocha huyo alisema Stars ilicheza vizuri kipindi cha kwanza kwa kuweza kuwadhibiti vizuri wachezaji wake lakini uzoefu uliwabeba hadi kuibuka na ushindi wa bao 2-0, mechi hiyo ilichezwa jana Jumamosi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

"Stars wana kikosi kizuri, walipambana sana ila kwangu Samatta ni bora zaidi anaonekana ana kitu cha ziada japokuwa alionekana kutoka mchezoni hasa baada ya kukosa penalti," alisema Kocha huyo.

Kwa upande wa Kocha wa Stars Charles Boniface Mkwasa alisema kukosa penalti kulipunguza morali kwa wachezaji na kuwa msaada kwa wageni kufanikiwa kupata bao la pili.

"Pamoja na Misri kuwa wazuri zaidi yetu lakini penalti ilitutoa mchezoni na kukubali kupoteza mchezo huo ambao ulikuwa muhimu kwetu," alisema Mkwasa.

Post a Comment

 
Top