BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu,
MABINGWA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga na timu nyingine zilizoshiriki katika msimu ulioisha wa 2015/16 zitakabidhiwa zawadi zao mapema mwezi ujao na Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania ambayo ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo.

 Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu alisema kuwa ucheleweshaji wa kutoa zawadi hizo umetokana na Yanga kushiriki  michuano ya kimataifa kama vile mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kuingia kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

 “Tunaomba radhi kwa  timu husika, wachezaji na wadau wa soka kwa zoezi hili kuchelewa ila tunawahakikishia kuwa  zawadi ziko tayari na zitakabidhiwa  mwezi ujao,” alisema Nkurlu.

 Pia Nkurlu alishukuru wadau wote waliofanikisha ligi hiyo hadi kufikia mwisho ambapo Yanga ya jijini Dar es Salaam iliibuka tena bingwa kwa mwaka huu.

 “Licha ya changamoto zinazoendeleza kujitokeza katika ligi yapo mafanikio makubwa na ligi hii inazidi kuwa na msisimko mkubwa nchini tunawashukuru wadau  wote na tuna imani kuwa itazidi kuwa bora katika siku za usoni,” alisisitiza Nkurlu.

Meneja huyo alisema kuwa Vodacom Tanzania itaendelea kutoa udhamini wa ligi hii msimu ujao kwa mujibu wa mkataba wake na TFF na aliwataka wadhamini wengine kujitokeza ili kuboresha zaidi ligi hii ikiwemo kuwawezesha wachezaji kunufaika zaidi katika ushiriki wake.

Post a Comment

 
Top