BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KAMPUNI ya Azam Media imeingia makubaliano ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mashindano ya Sports Extra Ndondo Cup kupitia Chanel ya Azam Sports HD yatakayoanza Jumapili Juni 5.

Mashindano hayo yataanzia katika hatua ya timu 32 ambapo mabingwa watetezi Faru Jeuri watafungua pazia dhidi ya Temeke Market katika uwanja wa Bandari huku bingwa wa michuano hiyo akiibuka na shilingi milioni 10.

Mkurugenzi mkuu wa Azam Media Rhys Torrington alisema wamechukua hatua hiyo ya kurusha mashindano ili kunyanyua soka la mchangani na kutoa fursa kwa vijana wengi kuonesha vipaji vyao.

Torrington aliongeza kuwa sasa muda muafaka wa Azam TV kuhamishia nguvu zake katika soka la mchangani wakianzia katika michuano hiyo iliyoanzishwa misimu miwili iliyopita.

"Tumedhamini Azam Confederation Cup, ligi kuu Tanzania bara, timu ya Taifa ya Wanawake na Sasa tumeibukia Ndondo Cup," alisema Torrington.

Nae Mkurugenzi wa vipindi vya Michezo Clouds FM, Shaffih Dauda alisema lengo la mashindano hayo ni kuendeleza soka la mitaani na kuvumbua vipaji vipya ambavyo vitaonekana katika nchi nyingi barani Afrika ambapo Azam inafika.

Post a Comment

 
Top