BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

UONGOZI wa klabu ya Yanga umekanusha vikali kuwepo kwa ugomvi baina ya washambuliaji  wake tegemeo Donald Ngoma na Amisi Tambwe.

Katikati ya juma lililopita kulisambaa taarifa kutoka nchini Uturuki ambako mabingwa hao waliweka kambi kuwa washambuliaji hao walipigana baada ya mabishano ya muda mrefu walipokuwa wanatoka mazoezini na kwamba Ngoma alizidiwa hoja jambo lililopelekea kupata hasira na kumvamia Tambwe.

Ofisa Habari wa timu ya Yanga Jerry Muro alisema kilichotokea ni majibizano ya kawaida mazoezini ndiyo wakakwaruzana lakini sasa hivi washambuliaji hao wapo vizuri na kambini hali ni shwari kabisa.

"Hakuna ugomvi baina ya Tambwe na Ngoma, walijibizana tu na baada ya hapo mwalimu aliongeanao huko huko Uturuki na hali iko shwari ndani ya kambi," alisema Jerry.

Taarifa za kuwepo kwa ugomvi baina ya washambuliaji hao tegemeo ziliibua taharuki miongoni mwa wapenzi na wanachama wa klabu hiyo kuelekea kwenye mchezo muhimu wa kombe la shirikisho dhidi ya TP Mazembe ambapo ingeharibu maandalizi ya timu na kupelekea kutofanya vyema.

Aidha Jerry amewataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kutosikiliza taarifa ambazo sio rasmi zinazoihusu Yanga badala yake wawasikilize viongozi wao.

"Taarifa hiyo imepotoshwa sana na Mimi ndiyo ninatoa taarifa rasmi kuwa hakuna 'bifu' lolote kati yao na wote wapo kambini tayari kuwasubiri Mazembe" alisema Jerry.

Post a Comment

 
Top