BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
NAHODHA wa timu ya Taifa ya  Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo katika mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu kombe la Mataifa Afrika dhidi ya Misri kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Samatta aliyejiunga na kambi ya timu hiyo kwenye Hoteli ya Urban Rose, iliyoko katikati ya jiji  nakufanya  mazoezi na wenzake kwenye Uwanja wa Taifa, aliwaambia waandishi wa habari na washindi wa promosheni ya Bia ya Kilimanjaro wanaodhamini timu hiyo kuwa shabiki ni mchezaji wa 12 katika kuleta hamasa ya ushindi na kuwatia nguvu wachezaji.

“Mimi ningependa kuwakaribisha mashabiki wote wa soka kuja uwanjani kwa ajili ya mchezo huu ili kutupa hamasa itakayotusaidia kupata ushindi,” alisema Samatta.

Samatta anayekipiga katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji atakuwa mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Misri kutokana na uwezo wake wa kucheka na nyavu.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa alisema kwamba kikosi chake kimekamilika na wachezaji wote wana ari  na hakuna mchezaji majeruhi anayeweza kukosa mchezo huo muhimu kwa Stars.

Tayari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)  limetangaza viingilio vya mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni kuwa ni Sh 5,000 na Sh 10,000.

Viingilio vilivyotangazwa ni Sh. 5,000 kwa mzunguko wenye viti vya Rangi ya Chungwa, Kijani na Bluu wakati Viti Maalumu vya alama 'B' na 'C' itakuwa ni Sh. 10,000.

Tiketi hizo zitauzwa kwenye vituo vya Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam, Ukumbi wa Burudani Mbagala Dar Live, vituo vya mafuta vya Oilcom - Ubungo na Buguruni (Buguruni Shell) na Ofisi za Ukumbi wa burudani Bilicanas.

Post a Comment

 
Top