BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys imeibuka na ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Shelisheli kwenye mchezo wa kufuzu michuano ya Afrika kwa vijana katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulikuwa wa upande mmoja ambapo Serengeti walitawala kwa muda mrefu na kufanikiwa kupata goli la kwanza dakika ya 15 kupitia kwa beki wa kushoto Nickson Clement baada ya mpira wa kona fupi uliopigwa na Asadi Ally.

Dakika sita baadae Ibrahim Abdallah aliipatia Serengeti goli la pili kufuatia mabeki wa Shelisheli pamoja na golikipa kushindwa kuondoa hatari katika lango lao na kumfanya mfungaji kuwa na kazi rahisi kutumbukiza mpira kimiani.

Serengeti waliendelea kulisakama lango la wapinzani na dakika ya 61 Ally Hussein alifunga goli la tatu kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji Mathew Bassot kunawa mpira alipokuwa akijaribu kuzuia shuti la mpira wa adhabu uliopigwa na Nickson Clement.

Baada ya goli hilo wageni walitumia muda mwingi kujiangusha na kupoteza muda baada ya kuzidiwa ujanja karibuni kila Idara na vijana wa Bakari Shime.

Serengeti iliwapumzisha Kelvin Nashon,Asadi Ally na Israel Patrick nafasi zao zikachuliwa na Enrick Vitalis, Cyprian Mtasigwa pamoja na Mohammed Rashidi.

Mwamuzi Belay Asserese hakuonesha kadi kwa mchezaji yoyote tangu kuanza kwa mtanange huo hadi mwisho.

Post a Comment

 
Top