BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
BAADA ya kuporwa wachezaji wawili waliokuwa wakitajwa kuwaniwa na Simba klabu hiyo sasa imehamisha mazungumzo yao kwa beki Salim Mbonde wa Mtibwa Sugar.

Awali Simba ilikuwa na nia ya kuwasajili kipa Beno Kakolanya wa Prisons pamoja na Andrew Vincent 'Dante' wa Mtibwa Sugar na tayari walifanya nao mazungumzo ya awali lakini wachezaji hao wawili jana walimwaga wino Yanga.

Beno na Dante walisaini mikataba ya awali ya miaka miwili kila mmoja na mara tu dirisha la usajili litakapofunguliwa watamalizana nao kabisa.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa mbali na Mbonde ambaye alikuwa kiongozi wa Dante katika kujenga ukuta wa Mtibwa,  pia watamrudisha beki wao Adam Miraji ambaye alikuwa akicheza Coastal Union kwa mkopo ila sasa mkataba wake umemalizika na ni mchezaji huru.


"Mbonde na Miraji ni wachezaji wazuri tu hivyo tunaamini watatufaa. Dante pia ni mzuri lakini tayari amesaini Yanga," alisema kiongozi huyo.

Kwa upande wake Miraji alisema: "Bado hatujakaa mezani rasmi ila kuna kiongozi mmoja amesafiri kasema akirudi atanitafuta hivyo nasubiri."

BOIPLUS inafahamu kwamba vigogo walioshikilia suala la usajili ndani ya Simba ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Collin Frisch ambao walikuwa Zimbabwe kwa ajili ya kufanya usajili wa straika.

Katika hatua nyingine Poppe amekaririwa akisema kiungo Justice Majabvi atakuwemo kwenye kikosi cha wekundu hao msimu ujao hivyo wapenzi na wanachama wa Simba wasiwe na hofu.

Post a Comment

 
Top