BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Dar
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetoa taarifa kwa maandishi kwa timu zote zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Ligi daraja la Kwanza ya StarTimes (FDL) msimu wa 2016/17 kwamba kila timu imetakiwa kuwasilisha jina la Uwanja ambao utatumia kama Uwanja wa nyumbani kabla ya Juni 20.

Wakati shirikisho hilo likiziandikia barua timu zote za VPL na FDL kuhusu uwasilishaji wa majina ya viwanja watakavyotumia kwa ajili ya mechi za nyumbani pia dirisha la usajili linafunguliwa kesho Jumatano.

Barua hiyo iliyotumwa kupitia Bodi ya Ligi (TPLB) ya TFF imeagiza jina la uwanja huo uende sambamba na taarifa za Vipimo vya uwanja, Iwapo unaweza kutumika kwa mechi za usiku au la, Idadi ya vyumba vya kubadilishia nguo ‘dressing rooms’, uwezo wa uwanja kuingiza mashabiki, mmiliki wa uwanja huo na aina ya nyasi (asili au bandia).

Barua hiyo imeelekeza kuwa iwapo timu haina uwanja wa nyumbani unaofaa kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom inaweza kuchagua uwanja mwingine katika mji au mkoa wa jirani. Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 6 (3) Ligi Kuu Tanzania Bara toleo la 2016/17.

Tayari TFF, lilitoa kalenda ya msimu mpya wa mashindano na matukio ambako usajili kuanza Juni 15 hadi Julai 30.

Kwa mujibu wa Kalenda hiyo, timu ambazo hazishiriki Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2016/2017 zitaanza kutangaza wachezaji walioachwa kuanzia Juni 15 hadi Juni 30.

Kwa upande wa timu zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), watatumia kipindi cha Juni 15 hadi Juni 30 kutangaza usitishwaji mkataba wa wacheaji. Usajili wao utaanza Juni 15 hadi Agosti 6.

Pingamizi itakuwa ni Agosti 7 hadi 14 kabla ya kuthibitisha usajili kwa hatua ya kwanza kati ya Agosti 15 na 19 wakati usajili hatua ya pili utaanza Agosti 17 hadi Septemba 7 na kitafuatiwa kipindi cha pingamzi hatua ya pili kuanzia Septemba 8 hadi Septemba 14, Septemba 15 hadi 17, itakuwa ni kipindi cha kuthibitisha usajili hatua ya pili.

Ratiba hiyo inasema kwamba timu zinatakiwa kuandaliwa  kuanzia Juni 15 hadi Julai 15,  ambako kuanzia Julai 16, hadi Agosti 14 ni kipindi cha mechi za kirafiki za ndani na nje. Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itatoka kati ya Julai 16 hadi Agosti 14.

Post a Comment

 
Top