BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MATUMAINI ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kucheza michuano ya AFCON itakayofanyika mwakani nchini Gabon yamefutika rasmi baada ya kukubali kichapo cha bao 2-0 dhidi ya Misri katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Stars ilianza mchezo huo kwa kasi huku dakika ya tisa Thomas Ulimwengu akipata nafasi ya kufunga lakini kichwa alichopiga kilitoka pembeni ya lango kabla ya Mbwana Samatta na Elius Maguli kupoteza nafasi pia.

Stars waliendelea kulisakama lango la wapinzani wao lakini Mapharao hao walianza kutikisa nyavu za Stars dakika ya 43 kupitia mchezaji wao  Mohammed Salah ukiwa ni mpira wa adhabu baada ya beki Haji Mwinyi kucheza faulo pembeni ya eneo la hatari.

Nahodha wa Stars, Samatta alikosa penalti dakika ya 53 baada ya Himid Mao kuangushwa ndani ya eneo la hatari na kupiga mkwaju uliopaa juu ya lango.Dakika ya 58, Salah alifunga goli la pili baada ya kupenyezewa pasi safi na Mohammed Elneny anayechezea Arsenal ya Uingereza.

Stars inabaki na pointi moja tu na kuburuza mkia katika kundi G ambapo imebakiwa na mchezo mmoja wa kukamilisha ratiba dhidi ya Nigeria utakaopigwa jijini Abuja, Septemba wakati Misri wao wameishafuzu.

Kocha wa Stars, Boniface Mkwassa aliwatoa Maguli, Haji na Ulimwengu nafasi zao zilichukuliwa na John Bocco,   Mohammed Hussein 'Tshabalala' pamoja na Deus Kaseke.

Katika mchezo wa awali uliofanyika nchini Misri mwezi Julai mwaka jana  Stars ililala kwa bao 3-0.

Post a Comment

 
Top