BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar

SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limesimamisha uchaguzi mkuu wa Klabu ya Stand United ya mjini Shinyanga baada ya kupokea barua mbili za uchaguzi wa klabu hiyo.

TFF ilipokea barua kutoka klabu ya Stand United na pia barua kutoka Kampuni ya Stand United Limited inayoongozwa na Mwenyekiti wao Amani Vincent huku Mkurugenzi akiwa ni Dr Jonas Tiboroha, jambo ambalo limekuwa likiwakanganya wadau wa soka.

Hata hivyo, TFF ilikwishabariki mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo unaosimamiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Stand United iliyobarikiwa na TFF, ambayo ilianza kazi yake Juni 13 chini ya wakili Paul Kaunda huku TFF ikieleza kwamba wanatambua klabu na sio Kampuni kwani ilikuwa haijakidhi vigezo vya kuwa kampuni.

Jana, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, aliwaandikia barua viongozi wa Stand United kusimamisha zoezi la uchaguzi wao unaotarajia kufanyika Juni 26 mjini Shinyanga, tamko ambalo limepingwa na viongozi wa Stand United na kwamba mchakato wao unaendelea na uchaguzi utafanyika siku iliyopangwa.

Wakati TFF ikisimamisha uchaguzi huo, tayari wadhamini wa klabu hiyo, Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia ulitoa siku 45 klabu hiyo iwe imefanya uchaguzi ili kupata viongozi watakaotambulika na kufanya nao kazi la sivyo watajitoa na mpaka sasa msimamo wao ni huo kwamba ifikapo Julai Mosi uchaguzi usipofanyika watajitoa.


Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA), 
Benester Lugola naye alikiri kupokea barua kutoka TFF ya kusimamisha zoezi la uchaguzi huo ingawa alionyesha kushangazwa na uamuzi uliotolewa na shirikisho hilo.

"Kweli nimepokea barua hiyo, ila nimeshangazwa na uamuzi huo maana ninavyofahamu mimi Kamati za uchaguzi za klabu zinakuwa kamati huru huwa haziingiliwi, tayari TFF waliipitisha hii kamati, iweje Katibu wa TFF ndiyo atoe uamuzi kama huo, ingekuwa kamati ya uchaguzi ndiyo inaahirisha kusingekuwepo na maswali yoyote.

"Unajuwa kinachopiganiwa ni kunusuru pia mdhamini asipotezwe maana muda aliotoa unakaribia kumalizika, uchaguzi usipofanyika Stand United haitakuwa na mdhamini tena, lakini ngoja tuone itakavyokuwa," alisema Lugola.

Kwa habari ambazo BOIPLUS imezipata kutoka ndani ya Stand United zinaeleza kwamba kesho Mwesigwa huenda akasafiri kwenda Shinyanga kwa ajili ya kikao cha pamoja kati ya viongozi wa klabu ya Stand United na wale wa Kampuni. 


Naye Katibu Mkuu wa wanachama waanzilishi wa klabu hiyo, Kennedy Nyangi alisema kuwa: "Viongozi wa TFF naona sasa wameanza kujichanganya wenyewe, wao ndiyo waliokuwa wanatuandikia barua kuhusu uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi kuibariki leo hii wananiandikia barua mimi kama Katibu mkuu, ni jambo la kushangaza.

"Tunamsubiri hiyo kesho ambayo amesema atakuja kwenye upatanisho, sijui anampatanisha nani wakati mwaka mzima walishindwa kupata suluhisho, uchaguzi unasimamiwa na Kamati za uchaguzi ya Stand United kwauangalizi wa Kamati ya uchaguzi ya TFF ambao hawajasema kitu chochote kuhusu uchaguzi wetu. Tunaendelea na mchakato wetu na hakuna kitakachobadilika na mchezo mchafu unaoendelea juu yetu hautafanikiwa, mpira hauendi kwa mfumo huu wanaotaka wao," alisema Nyangi

Hivi karibuni, TFF pia iliingilia uchaguzi mkuu wa Yanga lakini viongozi wa Yanga waliweka msisitizo kuwa wao ndiyo wenye mamlaka ya kupanga na kusimamia uchaguzi wao huku TFF wenyewe wana jukumu la kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani yaani ni waangalizi. TFF iliwabidi waitishe kikao cha pamoja na viongozi wa Yanga ili kuwaacha waendelee na mchakato wao.

Post a Comment

 
Top