BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea taarifa juu ya mpango na kauli za baadhi ya viongozi wa Yanga kushawishi mashabiki wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni ya moja kwa moja wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika ngazi ya Makundi dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo utakaofanyika Juni 28,  saa 10.00 jioni katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 TFF ikiwa msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, inawajibika na mara moja inachukua nafasi hii kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa Yanga, wanachama na mashabiki wao kutofanya hivyo kwani itakuwa ni kinyume na  kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini katika hatua hii.

 Ikumbukwe kwamba CAF inamiliki asilimia mia moja ya haki za habari na masoko katika ngazi hii ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya biashara au utengenezaji na urushaji wa matangazo ya televisheni au ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa CAF au wakala aliyeteuliwa na shirikisho hilo kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa faini tu bali pia uwezekano wa kuondolewa mashindanoni.

Pia TFF inatoa tahadhari hiyo ikiwamo ile ya utamaduni wa kukaa uwanjani ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye michezo yake hususani hii ya hatua ya makundi.

TFF inafahamu kuwa tayari viongozi wa Yanga walikwisha kusoma nyaraka na taarifa mbalimbali kuhusu kanuni na masuala ya udhamini kwa timu zinazofuzu hatua ya Nane Bora.Wapenzi wa Yanga wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu  timu yao ikiwa ni njia ya kuitia hamasa.Hata hivyo shamrashamra hizo zifanyike kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za Mpira wa Miguu na sheria za nchi.

Vitendo vya kuashiria vurugu na kufanya fujo vikithibitishwa katika taarifa ya Mwamuzi, Janny Sikazwe wa Zambia; Kamishna wa mchezo, Celestin Ntangungira wa Rwanda na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza, hatua zake zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo KUONDOLEWA KWENYE MASHINDANO. Vilevile vitendo vya kutishia amani,kudhuru mwili au kuharibu mali vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kijinai.

Post a Comment

 
Top