BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda
TIMU ya Taifa ya Misri imefuzu kucheza Fainali za mataifa ya Afrika baada ya kuifunga Taifa Stars mabao 2-0 jana katika dimba la Taifa. Kwasasa Stars inasubiri kwenda kucheza mechi ya kukamilisha ratiba tu dhidi ya Nigeria huku mafarao hao wakirejea nyumbani kupumzika.

Kumekuwa na mijadala kadhaa kwenye mitandao ya kijamii huku wachambuzi wa soka wakitoa maoni mbalimbali kuhusiana na mchezo wa jana. Wengi wamejaribu kutafuta mchawi, kila mmoja amemtaja wake lakini wengi wamesahau kuwa mchawi nambari moja ni uwezo mkubwa wa wachezaji wa Misri. Kwenye soka wale wenzetu walishakomaa miaka mingi sana iliyopita huku sisi tukiendelea 'kubeti' kwenye uchaguzi wa timu hadi upangaji wa vikosi.

Misri hawakuamka tu juzi na kuanza kujiandaa na mchezo dhidi ya Stars, maandalizi ya kile tulichokiona jana yalianza miaka mingi iliyopita na bado wanafanya mipango ya kujiandaa kufuzu AFCON na kombe la Dunia miaka kadhaa ijayo. Acha sisi tuendelee kuiwaza leo tu hata hatujui kesho atacheza nani Mbwana Samatta akistaafu.

Achana na hayo, kuna mambo ya kujiuliza lile somo la jana walilofundisha Mohamed Hussein 'Tshabalaa' na Deus Kaseke ada yake ni shilingi ngapi?, Ili ikalipwe pesa bila ubishi kwavile hakuna mmoja wetu ambaye hakuelewa. Kwani vijana hao wawili walikuja na mada zifuatazo;

1. BENCHI SI SEHEMU YA KUPIGA STORI, BALI KUUSOMA MCHEZO
Kabla Tshabalala na Kaseke hawajaingia, timu ilionekana kukosa hamasa huku wachezaji wakionekana wazi kukata tamaa. Haji Mwinyi ambaye alimpisha Tshabalala alionyesha kutojiamini baada ya kufanya makosa kadhaa huku Thomas  Ulimwengu aliyempisha Kaseke akidhihirisha kuzidiwa ujanja na wamisri ambao walijua mtindo wake wa kutumia nguvu kupenya katikati yao.


Wachezaji walioingia walitupa somo kuwa benchi ni mahali pa kujifunza kabla hujaingia kucheza. Tshabalala na Kaseke waliingia na utulivu mkubwa huku wakiachana na 'anao anao', waligongeana vizuri pasi fupi na kufanikiwa kuwahamishia mafarao katika eneo lao. Haya ndio mabadiliko ambayo kila mtu alikuwa akiyahitaji. Ilionyesha wazi kuwa walielewa nini wenzao walikosea kabla hawajaingia kurekebisha.

2. UMBO KUBWA LINA FAIDA, ILA SIO KILA KITU KWENYE MPIRA
Wakati wa mazoezi ya Stars ikiwa inajiandaa na mchezo wa jana,  Tshabalala alionyesha uwezo mkubwa kuliko Mwinyi, ila haikushangaza kuona kinda huyo mwenye nidhamu ya hali ya juu akiwekwa benchi katika mchezo huo. Kocha alishawishika zaidi na urefu wa Mwinyi hasa kwavile alijua angeenda kupambana na washambuliaji walioshiba.

Kila mmoja alijifunza kitu jana kuwa umbo kubwa pekee bila utimamu wa mwili kwa ajili ya mechi 'Match Fitness' ni kazi bure, Mwinyi alishindwa kuwazuia  washambuliaji wa Misri walioongozwa na mastaa Elneny na Mohamed Salah. Licha ya kufanana nao kimo bado wamisri hao walikuwa washindi kila mara kwenye mipira ya juu. 

Tshabalala yeye alijua udhaifu wake, akaamua kuepuka kukabiliana nao kwa kutumia nguvu, badala yake alikuwa akiingia miguuni na kupora mipira bila kusukumana nao. Baada ya muda wamisri wakagundua kuwa 'Chalii' huyo ni hatari kwao hasa alipopata moto na kuanza kuwashambulia, wakaamua kuanza kumkaba ingawa bado ilikuwa ngumu kwao kufanikiwa kutokana na ushirikiano wake mzuri na Kaseke.

3. 'HIGH RISK, HIGH RETURN'
Wazungu wanasema jilipue ufanikiwe. Kwa mchezo wa jana Kocha Boniface Mkwasa alipaswa ajilipue tu bila kutazama jina la mtu wala timu anayotoka. Kuna wachezaji wazoefu walionyesha kutokuwa vizuri tangu mazoezini huku wanaotajwa kutokuwa na uzoefu wakionyesha uwezo mkubwa.Wakati Elius Maguri anatoka, Stars ilikuwa inahitaji mtu mwenye kasi ili kuwaongezea presha Misri. Samatta ambaye alikuwa akizurura huku na kule kutafuta mipira na kutengeneza nafasi angeambiwa ajitulize mbele ya lango mahali ambapo alikuwepo Maguri. Halafu kama Kaseke angepewa nafasi, ni wazi kasi yake pamoja na ile ya Farid Mussa na Ulimwengu ingeweza kuzaa mabao kwavile sasa Samatta angekuwa ametulia jirani na lango. Na baada ya Ulimwengu kutoka, Shiza Kichuya angeweza kuwa wa msaada mkubwa.

Lakini sehemu nyingine ambayo Mkwasa alipaswa kujifunga mabomu na kufumba macho na masikio ni kwenye beki ya kushoto, Mwinyi hakustahili kuanza kwavile hakuwa 'fit' hata kidogo, kama kwenye klabu yake ya Yanga hakutumika kwa kipindi kirefu kwanini apewe nafasi kwenye kikosi cha timu ya Taifa?, kwanini asingemuanzisha Tshabalala ambaye licha kucheza vizuri katika mchezo dhidi ya Harambee Stars kule Kenya, alifanya vizuri mazoezini pia?. Aliohofia kujilipua, haya ndiyo matokeo ya hofu.

4. WALITUONYESHA 'PLAN B'
Mafarao walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kumiliki eneo la kati la uwanja licha ya jitihada zilizoonyeshwa na viungo wa Stars, Himid Mao na Mwinyi Kazimoto. Mwisho wa siku ilikuwa lazima timu ibadili mtindo wa kutafuta mabao.Kaseke na Tshabalala hawa naweza kusema ndio waliwafanya mashabiki wasijutie sana viingilio vyao, walifanya kila kilichohitajika ikabakia kufunga mabao tu. Kilichovutia zaidi ni kitendo chao cha kuja na 'Plan B'.

Kaseke alipoingia alienda upande wa kushoto hivyo Farid kulazimika kuhamia kulia alikokuwa akicheza Ulimwengu. Hii ilipelekea awe jirani na 'pacha' wake Tshabalala na kufanikiwa kuufanya upande wa kushoto kuwa ndio njia ya kulifikia lango la Misri badala ya katikati ambapo palizimwa kabisa.

Baada ya mpira kumalizika mashabiki waliamini kwmba endapo muda ungeongezwa zaidi basi Stars ingepata bao hata moja, hivyo ni wakati wa kulipa ada sasa juu ya elimu iliyotolewa na wachezaji hao.

Post a Comment

 
Top