BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa kamati ya uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF),  Wakili Aloyce Komba amejitoa kuratibu na kusimamia mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Yanga uliopangwa kufanyika Juni, 25 ambapo ameelezea sababu za kujitoa kwake.

Komba alitangaza sababu ambazo zimemfanya ajitoe kuwa ni kutuhumiwa kupanga kumhujumu kwa kukata jina la mgombea nafasi ya Mwenyekiti  Yusuf Manji, tuhuma ambazo zilitolewa jana Alhamisi mbele za waandishi wa habari.

Pili, Kombe alisema kutokana na tuhuma hizo, Manji alisema ni moja ya sababu zilizomfanya achukue fomu za kugombea uchaguzi utakaoratibiwa na Yanga.

"Tuhuma hizo ni kubwa kwangu binafsi na zinagusa taaluma yangu ya sheria zimetolewa wakati klabu ya Yanga inahitaji amani, utulivu na mshikamano mkubwa wa wanachama, wapenzi na washabiki wake, hivyo mimi kutokuwa chanzo chochote cha vurugu zinazoweza kutokea.

"Tuhuma hizo zinahusu mimi kupewa fedha za hongo au rushwa (kiasi hakijulikani) ili nishawishi wajumbe wenzangu wa kamati ya uchaguzi ya TFF kukata jina la mgombea, Manji kwasababu ambazo hazijaelezwa.

"Hivyo napaswa kupisha uchunguzi wowote huru wa tuhuma hizo nzito kama zimefikishwa katika vyombo vya uchunguzi wa masuala ya rushwa ili mimi nipate fursa ya kujitetea kwa uhuru zaidi," alisema Komba

Wakili huyo alisema kuwa kuzingatia ushauri wa watu mbalimbali nanaowaheshimu na kuwapenda  ndani na nje ya klabu ya Yanga hususani wanasheria wengine nguli wa masuala ya michezo kama vile Wakili Sais Hamad El-Maamry, Wakili Sam Mapande, Wakili Alex Mgongolwa na waandishi wa habari waandamizi wa michezo, ameona asishiriki mchakato huu kwa kusimamiwa na TFF au hata ukisimamiwa na klabu ya Yanga yenyewe.

"Kwakuwa mimi ni muumini mkubwa wa utawala wa sheria na hasa masuala ya katiba na demokrasia katika klabu na vyama vya michezo, napaswa kuanzia sasa kutoshiriki vikao vyote vinavyohusu mchakato wa klabu ya Yanga nikiwa kama Mwenyekiti au Mjumbe.

"Nawaomba Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu Mkuu Selestine Mwesigwa na wajumbe wenzangu wa kamati ya uchaguzi ya TFF, nimemuachia madaraka ya kuratibu na kusimamia uchaguzi wa klabu ya Yanga, Wakili Domina Mideli, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hii," alisema

TFF tayari ilianza kutoa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uchaguzi ndani ya Yanga wakati klabu hiyo ilianza kutoa fomu zao juzi na uchaguzi wao utafanyika Juni 11 huku Manji akiwafuta uanachama wagombea wote waliochukuwa fomu kupitia TFF.

Post a Comment

 
Top