BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Diamond Jubilee, Dar
KLABU ya Yanga imemaliza salama zoezi la kuchagua viongozi wake na sasa kinachoendelea ni zoezi la kuhesabu kura ambalo linakadiriwa kumalizika saa 4 usiku leo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Timu ya BOIPLUS ipo hapa kukupa  yale yanayojiri na hii hapa ni ripoti ya kwanza kabla matokeo kutangazwa rasmi na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo.

MAHUDHURIO
Maelfu ya wanachama walihudhuria uchaguzi huo ingawa kamati ilishindwa kutaja idadi kamili ya wanachama waliosajiliwa kwa ajili ya kupiga kura ingawa saa nane mchana kundi la wanachama kutoka mjini Morogoro liliwasili kwa Basi la kukodi  na kufanya idadi ya wapiga kura kuongezeka zaidi.Mgeni rasmi Raymond Mushi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala aliwasili ukumbini saa 5:30 asubuhi akifuatiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini Mama Fatma Karume, aliyewasili dakika tano baadaye. Mgombea pekee wa nafasi ya Uenyekiti katika uchaguzi huo, Yusuph Manji aliwasili ukumbini saa 6:12 mchana.

UHAKIKI WA WANACHAMA
Zoezi la uhakiki wa wanachama lilianza mapema ambapo kulikuwa na makundi mawili, wanachama wenye kadi za kawaida na wale wenye kadi zinazotolewa na Benki ya Posta.

Licha ya zoezi hilo kwenda kwa amani, baadhi ya wanachama wamelalamikia mtindo wa upatikanaji wa kadi za Benki ya Posta kwa madai kuwa ni rahisi kwa watu ambao si wapenzi wa Yanga kuzipata kwavile hakuna masharti yoyote yale zaidi kupigwa picha na kulipa pesa.

Katika uhakiki leo, walichokuwa wakikitazama maafisa wa Benki hiyo ni kama mwanachama amelipa ada na akionekana hajalipa basi Sh 12,000 ilikatwa kutoka katika akaunti yake na kuruhusiwa kupiga kura.

MANJI ATOA YA ROHONI
Alipopewa nafasi ya kujinadi, Manji alianza kuelezea mafanikio waliyoyapata katika uongozi wake uliopita huku akitaja makombe matatu waliyoweka kabatini kama mfano pamoja na kufuta 'uteja' kwa mahasimu wao Simba.

Akielezea suala la mechi za Yanga kuonyeshwa moja kwa moja na Azam TV, Manji alisema suala hilo limeiathiri kwa kiasi kikubwa timu yao hasa kushuka kwa mapato ya milangoni.

"Watu wengi sasa wanakaa vibandani na majumbani mwao kutazama mechi zetu, hawaendi uwanjani. Hata tukitaka kuuza jezi naamini mauzo yatakuwa chini kwavile sehemu nzuri ya kuvaa jezi ni uwanjani, sasa kama watu hawaendi unadhani watavalia wapi," alisema Manji.

Manji pia aliwaomba wanachama wachague wajumbe watakaoendana na msimamo wake wa kutowaingilia makocha na wachezaji katika kazi yao.

UPINZANI
Manji hakuwa na mpinzani katika nafasi ya Uenyekiti lakini Clement Sanga alibanwa mbavu na Titus Osoro ambaye anakitaka kiti cha Makamu Mwenyekiti. Hata hivyo wakati wakijinadi wagombea hao ilionekana wazi kuwa Sanga ana wafuasi wengi kuliko Osoro.

Kutokana na hilo matokeo yanayosubiriwa kwa hamu ni Makamu Mwenyekiti na wajumbe nane watakaounda kamati ya Utendaji ya Klabu hiyo.

WANACHAMA WACHANGIA UJENZI WA UWANJA
Katika hali ya kustaajabisha, baada ya mkuu wa Idara ya Habari na Mahusiano ya klabu ya Yanga, Jerry Muro kuzungumzia suala la Yanga kunyimwa kibali cha kujenga uwanja wao maeneo ya Jangwani, kundi la wanachama wa klabu hiyo liliinuka na kuanza kupeleka pesa meza kuu wakidai kama tatizo ni pesa zikalipwe wapewe kibali.

Pesa iliyokusanywa ilikadiriwa kufika Sh 1.3 milioni huku mama Karume akisema anaamini Rais John Pombe Magufuli ataona tukio hilo na kwamba litachukuliwa hatua kwa haraka. 

Akielezea jambo hilo, Mushi  alisema: "Hili jambo lipo kwenye mchakato, wataalamu wanaendelea kufanya vipimo katika eneo hilo ili kuhakikisha ujenzi huo hautaathiri mazingira, baada ya muda tutawapa taarifa kamili,''

Post a Comment

 
Top