BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda

WINGA wa Royal Eagles inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Afrika ya Kusini, mtanzania Uhuru Selemani alijiunga na timu yake juzi akitokea mapumzikoni, lakini akakutana na bonge la 'msala' mara baada ya kuwasili.

Akizungumza na BOIPLUS kutokea jijini Durban, nyota huyo wa zamani wa Coastal Union, Mtibwa na Simba alisema amepigwa faini ya dola 1,000 ambazo ni zaidi ya sh 2,000,000 kwa kosa la kushiriki michuano ambayo ndio 'habari ya mjini' kwa sasa, Sports Xtra Ndondo Cup bila ruhusa ya mabosi wake hao ambao walijua yupo nchini kwa ajili ya mapumziko tu.

"Wameniambia nilipe faini dola 1,000 baada kujua nilicheza mechi za Ndondo Cup, huku kuna ving'amuzi vinaonyesha Clouds TV kwahiyo walikuwa wanasubiri nifike tu hapa.

Lakini pia waliniona kwenye Azam HD wakati nacheza Ramadhan Cup pale Kidongo Chekundu, kwahiyo siwezi kukwepa adhabu hiyo. Hapa nataka niandike barua ya kuwaambia kuwa nilikuwa najiweka fiti tu ila wasiponisamehe itabidi nilipe hakuna jinsi," alisema Uhuru.

Uhuru aliichezea Temeke Market mechi tatu za Ndondo Cup na kufanikiwa kufunga mabao mawili huku kwenye Ramadhan Cup akiibuka mfungaji bora baada ya kuweka nyavuni mabao saba katika michezo mitano aliyoichezea Skywards FC.

Post a Comment

 
Top