BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

UONGOZI wa klabu ya Yanga umewapa mapumziko ya siku mbili Wachezaji wake baada ya kupoteza mchezo wake wa kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya TP Mazembe kwa goli 1-0 jana katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga itaingia kambini siku ya Ijumaa tayari kwa maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Medeama City utakaofanyika kati ya Julai 15 na 17 nchini Ghana ambapo ushindi pekee ndiyo utarudisha matumaini ya kusonga mbele kwa mabingwa hao wa Tanzania.

Ofisa Habari wa klabu hiyo Jerry Muro akizungumza mbele ya waandishi wa Habari alisema uongozi umeridhishwa na kiwango cha Wachezaji na benchi la ufundi huku ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika michezo ijayo.

"Uongozi unawapongeza Wachezaji kwa kujituma na kujitoa kwa ajili ya timu yao licha ya kufungwa na tumewapa mapumziko ya siku mbili kabla ya kurejea kambini kujiwinda dhidi ya Madeama," alisema Jerry.

Wakati huo huo Jerry alisema uongozi unawashukuru wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo waliojitokeza kwa wingi kushuhudia mchezo huo na wale walioshindwa kuingia uwanjani kutokana na kukosa nafasi kwa kuonesha mapenzi makubwa kwa Yanga na uzalendo.

Pia Jerry alisema kuwa kambi ya Dar es Salaam watakayoianza Ijumaa itakuwa ni ya muda mfupi kabla ya kutoka nje ya nchi ambapo alishindwa kuweka wazi mbele ya waandishi wa Habar kuwa watakwenda wapi.

Yanga imesalia na michezo minne, miwili nyumbani na mingine ugenini ambayo itabidi ishinde yote ili apate nafasi ya kuingia nusu fainali ya michuano hiyo.

Post a Comment

 
Top