BOIPLUS SPORTS BLOG

Na Mwandishi wetu, Dar

WAAMUZI wanne kutoka Ethiopia, ndio watakaochezesha mchezo wa kimataifa kati ya timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ na Shelisheli utakaofanyika Juni 26 saa 10.00 jioni katika Uwanja wa Taifa,jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ni wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17. Waamuzi hao ni Belay Tadesse Asserese ambaye ni mwamuzi wa kati wakati wasaidizi wake ni Tigle Gizaw Belachew upande wa kulia na Kinfe Yilma Kinfe upande wa kushoto huku mwamuzi wa akiba akiwa Lemma Nigussie, Kamishna wa mchezo huo atakuwa ni Bester Kalombo.

 Serengeti Boys ilikuwa kambini tangu Juni 14 kujiandaa na mchezo ambao watatakiwa kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa vijana.

Katika kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako ilishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) .

 Kadhalika Serengeti Boys ilicheza mfululizo michezo saba  ya kimataifa bila kufungwa dhidi ya Misri (2), India, Korea Kusini, Malaysia na Marekani (USA). Kabla ya hapo timu hiyo ilicheza michezo kadhaa ya ndani na timu za hapa nchini ikiwemo dhidi vya vijana wenye umri wa miaka 20 bila kupoteza.

Post a Comment

 
Top