BOIPLUS SPORTS BLOG

Wandishi Wetu

KLABU ya Simba inamshusha kocha Joseph Omog usiku wa leo kwa ajili ya kusaini mkataba na wekundu hao huku kocha  Jackson Mayanja akipewa nafasi kubwa ya kumrithi Adolf Rishard ndani ya Kagera Sugar.

 Habari  ambazo BOIPLUS  imezipata kutoka chanzo chake ndani ya Simba ni kwamba Mayanja amegoma kuwa msaidizi wa Omog kwa madai kuwa CV yake si ya kuwa chini ya kocha huyo raia wa Cameroon.

BOIPLUS pia ilimnasa kiongozi mmoja wa Kagera ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwenye mtandao huu akisema makocha Jackson Mayanja na Meck Mexime ndiyo wanaotajwa kuchukua mikoba huku Mganda huyo akipewa nafasi kubwa zaidi.

Mayanja aliwahi kukinoa kikosi hicho mwaka 2012 na kukifanya kuwa tishio kwa vigogo hasa wanapocheza katika uwanja wa Kaitaba na hii yaweza kuwa ndio sababu ya uongozi kutaka kumrejesha Mganda huyo.


"Uongozi unajidhatiti kuhakikisha wanairejesha timu kwenye mstari baada ya kuyumba sana na wataanzia katika benchi la ufundi" kilisema chanzo hicho.

Wiki iliyopita BOIPLUS ilizungumza na kocha Rishard kuhusu mustakabali wake ndani ya Wakata miwa hao akasema kila kitu atakiweka hadharani huku akionekana hakuwa na mazungumzo yoyote na mabosi wake.

Misimu miwili iliyopita Kagera ilikuwa miongoni mwa timu zilizokuwa zikitoa upinzani mkubwa kwa timu zinazoshiriki ligi kuu bara kabla ya kupitiwa na upepo mbaya na sasa wanataka kurejesha heshima yao.

Post a Comment

 
Top