BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar

MCHEZO wa hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho barani Afrika kati ya Yanga ya Dar es Salaam na TP Mazembe ya Lubumbashi DR Congo, umempa wakati mgumu straika wa KRC Genk Mbwana Samatta asijue dua zake azipeleke upande upi.

Samatta alikuwa straika tegemeo katika klabu ya Mazembe huku akiwa amedumu nayo kwa miaka minne kabla hajauzwa kwa vigogo hao wa soka nchini Ubelgiji ambao wamepata nafasi ya kushiriki michuano ya Europa msimu ujao wakianzia hatua ya awali.

Akizungumza na BOIPLUS kwa njia ya mtandao kutokea nchini Ubelgiji, Samatta alikiri kupata wakati mgumu kutoa msimamo wake kuelekea mchezo huo kutokana na mahusiano aliyonayo na timu hizo mbili.

"Mazembe pale nilishakuwa mwanafamilia, nimeacha marafiki wengi na kamwe siwezi kusahau mchango wao katika kufikia hapa nilipo, lakini si unajua tena Yanga ni timu ya nyumbani, ikifanya vizuri na soka la Tanzania linazidi kupata heshima Afrika na duniani kwa ujumla.

"Kwahiyo kuhusu hiyo mechi acha mimi niwe kimya tu, nawatakia mchezo mwema na wamalizane salama, najua utakuwa mgumu kwa pande zote mbili," alisema Samatta.

Yanga iliyopoteza mchezo wake wa kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria, inaikaribisha Mazembe kwenye dimba la Taifa katika mchezo utakaoanza majira ya saa 10 alasiri Juni 28.

Post a Comment

 
Top