BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar

MABINGWA wa Tanzania  timu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam imeianza vibaya michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika hatua ya makundi, baada ya kufungwa bao 1-0 na wenyeji wao Mo Bejaia ya nchini Algeria usiku wa kuamkia leo.

Ni wazi Yanga ilijiandaa kisayansi kuingia katika mchezo huo na kwamba matokeo hayo yametokana na kuzidiwa mbinu tu na waarabu hao ambao hawakuonyesha kiwango cha kutisha sana, hawajapoteza kutokana na ufinyu wa maandalizi.

Kwa kujua hali ya hewa ya Algeria kuwa ni baridi, Yanga waliamua kwenda kuweka kambi nchini Uturuki ambako kuna baridi pia huku wakifanya mazoezi usiku, muda sawa na ule ambao mechi ilipangwa kuchezwa, haya ndio maandalizi ya kisayansi.


Timu nyingine za Tanzania zinapaswa kujifunza aina hii ya maandalizi ili kufikia mafanikio. Ni ajabu kwa timu inayojiandaa kwenda kucheza nchi za ukanda wa joto iweke kambi sehemu yenye baridi. Huko ni kubeba maparachichi Dar na kwenda kuyauza Mbeya.

Yanga sasa inajiandaa na mchezo wa pili dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa jijini Dar Juni 28. Nilishtuka nilipopokea taarifa kuwa timu hiyo inaanza safari ya kurejea Uturuki katika mji wa Antalya kuendelea na kambi yake, nikajiuliza 'Yanga wamesahau nini tena Uturuki?'

Kocha yoyote anapenda mazingira tulivu ili aweze kuhakikisha mafundisho yake yanawaingia vizuri wachezaji, hii yaweza kuwa sababu kubwa iliyowafanya  Wababe hao wa mitaa ya Twiga na Jangwani wanogewe na kambi ya Antalya, lakini wamejiuliza kuhusu hali ya hewa?


Sidhani kama ni sahihi kwa Yanga kuendelea na kambi ya Antalya wakati wanajua hali ya hewa ya kule ni tofauti kabisa na ya Dar ambako mchezo utafanyika. Nilitarajia Yanga wangerejea nchini na katika kutafuta utulivu basi wangekimbilia hata kisiwani Pemba ambako huwa hakuwaangushi.

Licha ya mwezi mtukufu wa Ramadhan, Pemba panabaki kuwa sehemu tulivu na sahihi zaidi kwa Yanga kuelekea kuwavaa Mazembe ambao wenyewe wameanza vizuri michuano hiyo kwa kuifumua Medeama mabao 3-1 jijini Lubumbashi.

Acha nijifariji kuwa Yanga watapumzika  tu pale Antalya kwa siku moja kabla hawajaanza safari ya kurejea nchini, hawatoweka kambi kama ilivyoelezwa kwavile kufanya hivyo ni kujiongezea ugumu wa mechi.

Post a Comment

 
Top