BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Dar
NDANI ya siku moja mabingwa wa Ligi Kuu Bara Yanga wamefanya ukatili mkubwa kwa watani zao Simba baada ya jioni hii kumnasa beki Vincent Andrew 'Dante' kutoka Mtibwa Sugar.

Asubuhi ya leo, Yanga walimpa mkataba wa miaka miwili kipa wa Prisons, Beno Kakolanya, wachezaji wote wawili walikuwa kwenye rada za usajili kwenye kikosi cha Simba.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro zimethibitisha juu ya usajili huo na kwamba sasa hao ni mali halali ya Yanga na kuwafanya Simba waanze kukuna upya vichwa vyao kupata wachezaji wengine.

Wachezaji hao wamesaini mikataba hiyo wakiwa wachezaji huru baada ya mikataba yao ya ajira katika timu zao kumalizika na kuamua kwenda kupata changamoto mpya.

"Leo tumesajili wachezaji wawili Dante na Kakolanya na bado tunaendelea kuimarisha kikosi hivyo mashabiki na wanachama wasubiri kupata mambo mazuri zaidi," ilisema Muro.

Taarifa za ndani ya Simba zinadai kuwa sio kweli kwamba wameporwa Kakolanya, bali waliamua kuachana naye baada ya 'kutonywa' na wanazi wao waliopo jijini Mbeya kuwa kipa huyo asingewafaa.

Post a Comment

 
Top