BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma,Dar
SIKU moja baada ya Baraza la Michezo Tanzania BMT kutangaza kuendelea na mchakato wa uchaguzi wa klabu ya Yanga, Uongozi wa klabu hiyo umeibuka na kutaja tarehe rasmi ya uchaguzi huo.

Katibu mkuu wa klabu hiyo Deusdedit Baraka ametangaza Juni 11 kuwa ndiyo uchaguzi utafanyika huku fomu za kugombea zikianza kutolewa leo.

BMT iliiandikia barua klabu hiyo kufanya Uchaguzi Juni 25 lakini uongozi wa Yanga umerudisha nyuma tarehe hiyo kwa wiki mbili.

Baraka pia alisema Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo ndiyo itasimamia suala zima la uchaguzi na shirikisho la mpira wa miguu TFF halina mamlaka ya kuingilia mchakato huo.


"Jana wametangaza kutoa fomu kwa wagombea sasa hao TFF wana rekodi gani ya wanachama wa klabu ya Yanga, wana uhakika kuwa hao waliochukua ni wanachama halali wa Yanga," alihoji Baraka.

Pia katibu huyo alitolea ufafanuzi juu ya kadi za kupigia kura kama zitakuwa ni zile za zamani au mpya "Kadi za zamani na zile za posta zote ni halali na zitatumika katika uchaguzi huu" alisisitiza Baraka.

Aidha Katibu huyo alisikitishwa na kauli ya Mwenyekiti wa kamati ya Uchaguzi ya TFF  Wakili Aloyce Komba kuwa uongozi wa klabu hiyo ni batili kutokana na kukiuka katiba yao ya kutofanya Uchaguzi kwa mwaka mmoja na nusu.

"Kama uongozi ni batili basi mataji tuliyochukua pia ni batili, Na kwanini wanatuandikia barua ya kushiriki masuala mbali mbali katika kamati ya Utendaji ndani ya TFF," alimalizia Baraka.

Post a Comment

 
Top