BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu, Dar
BAADA ya kuibuka na ushindi wa magoli 6-0 dhidi ya Polisi Morogoro kikosi cha timu ya Simba sasa kimewapa kiburi nyota wake kuwa mambo yanakwenda vizuri kuelekea mikikimikiki ya ligi kuu msimu mpya.

Simba ambayo imeweka kambi mkoani Morogoro kwa ajili ya maandalizi ikiwa chini ya kocha Mcameroon Joseph Omog imepania kurejesha makali yake ambapo kwa sasa inaonekana kutia moyo.

Mshambuliaji wa timu hiyo Ibrahim Ajib ameiambia BOIPLUS kuwa kwa sasa kikosi cha Simba kiko vizuri kutokana na kuongezwa kwa nyota muhimu kadhaa toka timu mbali mbali.

"Kiukweli kabisa tuna kikosi kizuri na tuna uwezo mkubwa kuchukua ubingwa msimu ujao, kwa kikosi hiki tu kilichosajiliwa tunaweza kufanya makubwa," alisema Ajib.

Miezi michache iliyopita mshambuliaji huyo alikwenda kufanya majaribio katika klabu ya Golden Arrows inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Afrika Kusini bila kuaga uongozi wa Simba.

Tayari Simba imewasajili wachezaji Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim,Muzamir Yassini, Jamal Mnyate ambao kiwango chao mazoezini na katika mchezo wa juzi kimeonyesha wanaweza kuisaidia Simba msimu huu.

Simba itafungua ligi na Ndanda FC katika mchezo utakaofanyika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam Agosti 20.


Wakati huo huo wekundu hao wa Msimbazi wamemshusha straika Diawuo Johnson kutoka Ghana kwa ajili ya kufanya majaribio na kama akifuzu basi atakuwa mmoja wa watakaotambulishwa Simba Day.

Post a Comment

 
Top