BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar
RAIS wa Simba Evance Aveva amefunguka mbele ya wanachama wa klabu hiyo kuwa uongozi wake uliboronga kwenye usajili wa wachezaji kutoka nje ya nchi msimu uliopita.

Aveva aliyasema hayo leo kwenye mkutano mkuu alipokuwa akiwasilisha taarifa kutoka Kamati ya Utendaji juu ya uendeshaji wa klabu hiyo kwa msimu wa 2015/16.

Rais huyo aliuambia mkutano mkuu kuwa wachezaji wengi wa kigeni waliosajiliwa msimu uliopita walikuwa wa viwango vya chini na hawakustahili kuichezea Simba.

"Tunakiri kuboronga katika  usajili wa wachezaji wa kigeni, ni wazi usajili haukuwa makini na kwamba tulizitumia vibaya nafasi saba tulizopewa," alisema Aveva.

Katika hatua nyingine Aveva alisema matokeo mabaya ya Simba msimu uliopita yalitokana pia na kuwepo kwa wachezaji wasaliti katika kikosi hicho akitolea mfano wachezaji waliogoma kwenda Songea kwa madai ya kutolipwa mishahara yao.

"Tuligundua katika jeshi letu la msimu uliopita kulikuwa na wanajeshi wenye wasaliti, mshahara wa Simba unalipwa tarehe nane ilikuaje wachezaji wagome tarehe nane hiyo hiyo?," alihoji Aveva.

Mkutano mkuu wa wanachama unaendelea katika Ukumbi wa Police Officers' Mess na wanachama wengi wanasubiri kwa hamu ajenda namba tisa inayozungumzia mfumo wa uendeshaji.

Post a Comment

 
Top