BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KIKOSI cha timu ya Ndanda ya mkoani Mtwara kitasafiri kesho kuja jijini Dar es Salaam kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya ligi kuu Tanzania bara itakayoanza Agosti 20.

Ndanda imeondokewa na kocha wake Malale Hamsini aliyejiunga na JKT Ruvu baada ya kugoma kuongeza mkataba kutokana na kushindwa kufikia makubaliano ya kuboresha mkataba wa awali.

Katibu mkuu wa timu hiyo Selemani Kuchele ameiambia BOIPLUS kuwa wapo katika mchakato wa kutafuta kocha mkuu kwa ajili ya kuendelea na programu za mazoezi kuelekea kufunguliwa kwa pazia la ligi kuu mwezi ujao.

"Timu itasafiri kesho kuelekea Dar huku tukiwa katika harakati za kutafuta kocha mkuu haraka ili ajiunge na kikosi tayari kwa maandalizi ya ligi mwezi ujao"alisema Kuchele.

Aidha Katibu huyo alisema kocha ambaye atajiunga na Wanakuchele hao atakuwa ni kocha mzawa ambaye watamuweka wazi siku chache zijazo.

Katika hatua nyingine Kuchele alisema kuwa hawajamsajili kiungo wa zamani wa klabu ya Yanga Salum Telela ila habari zinapotoshwa juu ya mchezaji huyo tangu mkataba wake ulipomaliza na vijana wa Jangwani.

"Hakuna ukweli wowote kuhusu Telela kusajiliwa nasi ni maneno tu ya mtaani ila muda ukifika tutatangaza wachezaji wetu tuliowasajili na tuliowaacha,"alisema Kuchele.

Post a Comment

 
Top