BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MATUMAINI ya mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika yamezidi kufifia baada ya kulazimishwa sare ya goli 1-1 na Medeama FC kutoka Ghana katika mtanange uliofanyika kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Dakika ya kwanza tu ya mchezo mshambuliaji Donald Ngoma aliipatia Yanga goli baada ya kupokea pasi safi toka kwa Thaban Kamusoko lakini furaha yao ilidumu kwa dakika 14 pekee kufuatia Bernard Danso kuisawazishia Medeama kwa goli la kisigino kutokana na mpira wa kona ambao mabeki walishindwa kuokoa.

Medeama walionekana kuwa wazuri kutokana na kucheza kwa ulewanao mkubwa kuanzia nyuma, kati hadi mbele ambapo walikuwa imara zaidi na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga huku Yanga wakikosa mbinu za kuwapenya.


Kipa wa Medeama Daniel Agyei

Dakika ya 47 mshambuliaji Amissi Tambwe alikosa goli la wazi akibaki na mlinda mlango Daniel Agyei na mpira wake kupanguliwa kabla ya mabeki wa Medeama kuondoa katika hatari.

Kamusoko alipiga shuti Kali langoni mwa Medeama lakini mlinda mlango Agyei alipangua na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Yanga waliendelea kutengeneza nafasi za kufunga huku mchezaji Juma Mahadhi ambaye aliingia dakika ya 75 akionesha uwezo mkubwa licha ya kucheza dakika chache.

Yanga iliwatoa Tambwe, Oscar Joshua nafasi zikachuliwa na Mahadhi pamoja na Haruna Niyonzima. Medeama waliwatoa Paul Aidoo, Enock Agyei nafasi zao zikachukuliwa na Salufu Moro na Malik Akowuah.

Yanga inaendelea kuburuza mkia katika kundi A baada ya kupata alama moja huku Medeama wakiwa nafasi ya tatu wakiwa na pointi mbili.

Post a Comment

 
Top