BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KOCHA mpya wa timu ya Majimaji ya mkoani Ruvuma Hassan Banyai amekiri kuwa atakuwa na kazi ngumu kuandaa kikosi chake baada ya kuondokewa na nyota  kadhaa wa kikosi cha kwanza.

Wachezaji hao  ni pamoja na golikipa David Burhan na beki Godfrey Taita waliojiunga na Kagera Sugar pamoja na mshambuliaji Danny Mrwanda ambaye mkataba wake umeisha.

Banyai ni miongoni mwa makocha walioanza kozi ya leseni A ya Ukocha inayotolewa na shirikisho la mpira wa miguu barani Afrika CAF iliyofunguliwa na Rais wa TFF Jamal Malinzi mapema hii leo katika ofisi zake zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam.

Banyai ameiambia BOIPLUS kuwa tayari ameshapeleka mapendekezo ya wachezaji anaowahitaji huku akisema anajitaji marekebisho makubwa karibuni kila idara ya kikosi hicho cha Wanalizombe.

"Kama unavyoona hata kipa kaondoka kwahiyo tunatakiwa tupate wachezaji wazuri kila idara kuanzia mabeki,viungo hadi washambuliaji ili tuwe washindani wa kweli katika ligi inayoanza mwezi ujao" alisema Banyai.

Banyai anachukua mikoba iliyoachwa na kocha Kali Ongala ambaye amemaliza kandarasi na Wanalizombe hao mwishoni mwa msimu uliopita na kufanikiwa kukinusuru kikosi hicho na janga la kushuka daraja.

Msimu mpya wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara unaotarajiwa kuanza mwezi ujao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na maandalizi yanayofanywa na timu shiriki kuanzia kwa makocha hadi kwa wachezaji.

Post a Comment

 
Top