BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MWANAMUZIKI Emanuel Elbariki 'Ney Wamitego' amefungiwa kujihusisha na masuala ya muziki kwa muda usiojulikana pamoja na kulipa faini ya shilingi milioni moja baada ya wimbo wake unaoitwa ‘Pale kati patamu’ kukosa maadili.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania BASATA, Godfrey Mngereza alisema katika wimbo huo Ney ameimba matusi ambayo kwa mujibu wa tamaduni za kiafrika ni jambo ambalo haliwezi kuvumilika.

"Mwanamuziki Ney Wamitego amefungiwa kujihusisha na masuala ya muziki kwa muda usiojulikana pamoja na faini ya milioni moja kutokana na wimbo wake wa 'Pale kati patamu kukosa maadili" alisema Mngereza.

Kwa upande wake Rapa Ney Wamitego alisema ana kazi nyingi za kufanya licha ya kukiri kuwa mziki ndiyo uliokuwa akiutegemea kwa kumuingizia kipato chake cha kila siku.

Ney pia alisema hata kama amefungiwa lakini wimbo wake umefanya vizuri katika vituo mbali mbali vya radio na luninga huku ujumbe aliutaka kufika kwa walengwa.

"Tayari Ujumbe ulishawafikia  watu, nitafanya mambo mengine sina wasiwasi na kufungiwa kwangu" alisema Ney.

Hii sio mara ya kwanza kwa rapa huyo kufungiwa kwani miezi michache iliyopita wimbo wake wa 'Shika adabu yako' ulisitishwa kupigwa katika vituo mbali mbali vya habari na Basata kutokana na maudhui yake.

Post a Comment

 
Top