BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda

BEKI wa kushoto wa Neckarsulm Sport Union inayoshiriki ligi daraja la tano nchini Ujerumani, mtanzania Emily Mgeta usiku wa kuamkia leo amenusurika kifo baada ya kupata ajali mbaya ya gari katika mji wa Neckarsulm

Mgeta ambaye alianza kung'ara na kikosi cha pili cha wekundu wa Msimbazi Simba alikuwa na rafiki zake wawili wakitoka kutazama mchezo wa nusu fainali ya kombe la EURO 2016 kati ya wenyeji Ufaransa na Ujerumani mchezo uliomalizika kwa Ujerumani kubamizwa mabao 2-0.

Ajali hiyo ambayo ilitokea wakiwa wanarejea mjini Heilbronn wanakoishi, ilisababisha kifo cha dereva Illia Kerlos mwenye asili ya Ukraine ambaye ni rafiki mkubwa wa Mgeta huku yeye mwenyewe na mwenzake mmoja wakinusurika.


"Namshukuru Mungu na siamini kama nimetoka nikiwa hai, gari ilipinduka mara mbili baada ya kuhama njia na kugonga ukingo wa barabara.

"Nasikia maumivu makali ya mbavu na kichwa ila nimepimwa wameniambia si tatizo kubwa sana, ni kutokana na kujigonga wakati gari linapinduka," alisema beki huyo ambaye amejihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha wajerumani hao.

Mgeta alitibiwa usiku huo huo na kuruhusiwa kurejea nyumbani huku rafiki yake mmoja akibakia hospitali kwa matibabu zaidi.

Post a Comment

 
Top