BOIPLUS SPORTS BLOG

Zainabu Rajabu, Dar
BAADA ya kuenea kwa uvumi kuwa kiwango cha nahodha wa Azam FC John Bocco 'Adebayor' hakijamfurahisha kocha Mhispania Zeben Hernandez, uongozi wa timu hiyo umefunguka kuwa huo ni uzushi na nyota huyo ataendelea kuwepo kikosini.

Akizungumza na BOIPLUS katika mahojiano maalum Ofisa Habari wa Azam Jaffar Iddi Maganga alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote na kocha Hernandez amekiri kumhitaji katika mipango yake.

"Taarifa hizo hazina ukweli wowote Bocco ni nahodha wetu na ataendelea kuwepo ndani ya kikosi,tunahitaji huduma yake na imani yetu atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaovaa jezi ya Azam msimu ujao," alisema Maganga.

Aidha Maganga aliongeza kuwa kama kungekuwa na msuguano wowote baina ya nahodha huyo na kocha wake basi Mhispania huyo asingekataa ofa ya Bocco kutakiwa na klabu moja nchini Morocco.

"Tulipokea ofa ya Bocco kutoka klabu moja nchini Morroco lakini kocha Hernandez alikataa tusimuuze, sasa kama angekuwa hamtaki si angeacha tumuuze" alisema Jaffar.

Wakati huo huo Jaffar amejinasibu kuwa msimu huu unaotarajiwa kuanza Agosti 20 wana nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa kutokana na ubora wa kikosi chao.

Post a Comment

 
Top