BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KUKOSEKANA kwa beki Vicent Bossou katika mchezo wa marudiano wa kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya Medeama ya Ghana kumeigharimu Yanga kwavile kulisababisha kutokuwepo kwa utulivu kwenye idara ya ulinzi.

Hayo yalisemwa na kiungo wa zamani wa klabu hiyo Ally Mayai alipozungumza na BOIPLUS  leo huku akiongeza kuwa kuwa licha ya wachezaji wote kutokuwa katika kiwango bora, pengo la Bossou limechangia kwa kiasi kikubwa zaidi kupoteza mchezo huo.

"Idara ya ulinzi ilifanya makosa mengi hii inatokana na ubora wa wapinzani ila kutokuwepo kwa Bossou ilikuwa pengo kubwa na kulazimishwa kufanya makosa mengi yaliyopelekea kupoteza mchezo," alisema Mayai.

Aidha Mayai alisema pia Mbuyu Twite alicheza vizuri katika nafasi ya kiungo mkabaji ila tatizo kubwa lilikuwa ni kupandisha timu wakiwa na mpira kitu kilicho sababisha kukosekana kwa muunganiko na kuwapa mwanya wapinzani.

Kiungo huyo pia alisema Yanga ndiyo timu ambayo inatoka katika nchi iliyo chini katika viwango vya ubora katika timu zote za kundi A licha ya Watanzania wengi kuamini kuwa mabingwa hao wapo katika hali sawa na wapinzani wao.

"Angalia hata katika viwango vya soka Tanzania tupo chini huwezi kutulinganisha na Algeria,Ghana wala DR Congo kwahiyo Yanga ilikuwa na nafasi finyu ya kupenya katika kundi hilo" alisema Mayai.

Bossou alikosa mchezo huo baada ya kuwa na kadi tatu za njano alizozipata katika mechi dhidi ya TP Mazembe na Medeama zilizofanyika katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam na ile Mo Bejaia.

Kocha wa Yanga Mholanzi Hans van Pluijm aliwapanga mabeki Kelvin Yondani na Nadir Haroub ambao walishindwa kuhimili vishindo vya wenyeji kwa kufanya makosa ya mara kwa mara yaliyopelekea kupoteza mchezo huo kwa kukubali kichapo cha magoli 3-1.

Post a Comment

 
Top