BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar

TIMU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam ilipoteza mchezo wake wa pili wa kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe kwenye uwanja wa Taifa siku ya Jumanne. Kabla ya hapo ililazwa bao 1-0 na MO Bejaia nchini Algeria.

Matokeo hayo yamewakatisha tamaa wapenzi na wanachama wengi wa klabu hiyo hasa kwavile waliamini wangeweza kuutumia vema uwanja wao wa nyumbani na kuibuka na ushindi wa kwanza. Baada ya mchezo huo maelfu ya mashabiki waliovalia jezi za njano na kijani walionekana kukosa amani huku wakitoka uwanjani kwa unyonge

Mpira ni mchezo wa makosa, Yanga walifanya kosa Mazembe wakalitumia kupata pointi tatu, Mazembe walifanya makosa lakini Yanga hawakuyatumia kuwaadhibu, matokeo yake ndiyo kupoteza mchezo.

Licha ya matokeo hayo, bado Yanga ina nafasi ya kufuzu hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho na hapa BOIPLUS inakuletea maelezo ya jinsi gani vijana hao wa Jangwani wanaweza kufuzu.

KUSHINDA MECHI TATU TU

Yanga imebakiwa na michezo minne ili kumaliza hatua hii ya makundi, ili kucheza nusu fainali Yanga wanapaswa kufanya maombi ya kutosha wakati huo huo wakihakikisha wanashinda japo mechi tatu tu kati ya hizo nne zilizo kibindoni.

Kwa mtindo wowote ule Yanga watalazimika kuzifunga Mo Bejaia na Medeama zitakapokanyaga nyasi za uwanja wa Taifa huku wakiandaa sumu ya kwenda kuwaua kwao aidha TP Mazembe au Medeama. Wakifanikiwa katika hilo watakuwa wamejizolea pointi tisa.

KUIOMBEA MEMA MAZEMBE

Hapa hakuna namna, licha kufungwa na wakongo hao ni lazima Yanga wageuke kuwa mashabiki wa Mazembe huku wakiwaombea mema kwenye michezo yao iliyosalia.Ni ngumu kuizuia Mazembe yenye pointi sita isicheze nusu fainali, kwahiyo ni bora kuiombea mema tu ikibidi hata kushinda dhidi ya Yanga yenyewe kwenye mchezo utakaopigwa jijini Lubumbashi.

Yanga wanapaswa kuwaombea Mazembe wapate japo sare katika mechi zake za ugenini dhidi ya Mo Bejaia na Medeama huku wakiifunga Bejaia nyumbani Lubumbashi.

Kama itakuwa hivyo maana yake ni kwamba Mazembe watamaliza katika nafasi ya kwanza kwa kukusanya pointi 14 huku pia wakiwa wamewadhoofisha Bejaia na Medeama ambao ndio washindani wa Yanga kwenye kuisaka nafasi ya pili.

MO BEJAIA, MEDEAMA ZITOKE SARE
Kama dua ya kuiombea Mazembe ipate matokeo mazuri dhidi ya Bejaia na Medeama itapokelewa, baada ya hapo dua nyingine inatakiwa iwe kwa timu hizi mbili zitakapokutana katika mchezo wa pili ziambulie sare.

Tayari Bejaia wamejizolea pointi nne baada ya kuifunga Yanga na kulazimisha sare nyumbani kwa Medeama. Kama watapata sare katika mechi mbili (dhidi ya Mazembe na ile dhidi ya Medeama nchini Algeria) huku pia ikipoteza mechi za ugenini dhidi ya Mazembe na Yanga, basi watafikisha pointi sita tu hivyo kutoifikia Yanga ambayo kwa mujibu wa mahesabu hapo tayari itakuwa na alama tisa.


Kama mambo yatakwenda hivyo Yanga itaungana na Mazembe kufuzu nusu Fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa katika ngazi ya klabu barani Afrika. 

Huu hapa ni msimamo utakavyokuwa kama dua za Yanga zitapokelewa;

                          P     Pts
1. TP Mazembe    6      14
2. Yanga             6        9
3. Mo Bejaia        6        6
4. Medeama        6        3

Post a Comment

 
Top