BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
MKUU wa kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga Jerry Muro ameutaka uongozi wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF kumuomba radhi kwa kumdhalilisha baada ya kumuandikia barua ya malalamiko ya kumtaka kwenda kwenye kamati ya maadili.

Akiongea kwa masikitiko mbele ya waandishi wa Habari katika makao makuu ya klabu hiyo, Jerry alisema kuwa TFF walipaswa kuwaandikia barua Yanga ambao ndio mwanachama wao na si yeye kwa mujibu wa katiba ya nchi.

TFF ilitoa tamko jana kupitia kwa Ofisa Habari wake Alfred Lucas ya kumuita Jerry mbele ya kamati ya maadili ya shirikisho hilo kutokana na maneno ya kichochezi aliyoyatoa mbele ya waandishi wa Habari siku chache zilizopita.

"Mimi sio mwanachama wa TFF, nimeajiriwa na Yanga kwahiyo kama kuna nililofanya ilibidi waiandikie klabu sio mimi, ila itajulikana mbivu na mbichi," alisema Jerry.

Jerry anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo kesho Julai 2 katika ofisi za TFF saa 4 asubuhi kwa ajili ya kusikiliza shauli hilo ambalo alisema atafika bila kukosa.

"Wapenzi na wanachama wa Yanga wamekuwa wakiniuliza kuwa nitahudhuria au la, kiukweli kesho nitaenda kuwasikiliza wanachotaka ili ijulikane mbivu na mbichi" alisema Jerry.

Aidha Jerry aliwatahadharisha viongozi hao wa shirikisho wakiongozwa na Rais Jamal Malinzi kuwa wasipokuwa makini suala hilo litawafikisha pabaya.

Post a Comment

 
Top