BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi,Dar
KOCHA wa Mwadui FC (Leicester City ya Bongo) Jamhuri Kihwelo 'Julio' amejinasibu msimu huu hakuna timu itakayomfanya ashindwe kuchukua ubingwa wa ligi kuu Vodacom Tanzania bara.

Julio amefanya marekebisho makubwa katika kikosi chake kwa kuwaacha wachezaji wakongwe kama Athumani Iddi, Nizar Khalfan, Razack Khalfan, Malika Ndeule pamoja na Kelvin Sabato huku akiwaongeza wachezaji vijana akiwemo Abdala Seseme aliyekuwa akicheza Toto Africa.

Kocha huyo mwenye maneno mengi pamoja na timu yake  wapo kambini jijini Dar es Salaam ambapo wanafanya mazoezi katika viwanja vya Leaders kwa ajili ya kujiwinda na msimu mpya wa ligi utakaoanza Agosti 20.

Julio alisema kuwa wameamua kuja kuweka kambi jijini Dar es Salaam ili iwe rahisi kwa wao kupata mechi za kujipima ubavu baada ya timu nyingi zinazoshiriki ligi kuu kuwepo hapa kama Mtibwa, Ndanda na Kagera Sugar.

"Dar ndo kila kitu hapa nchini, kuna viwanja vizuri vya mazoezi na wenzetu wengi wapo huku kwahiyo itakuwa rahisi kwetu kupata mechi za kirafiki," alisema Julio.

Aidha kocha huyo aliuponda utaratibu wa baadhi ya timu kuleta wachezaji wa kimataifa kufanya majaribio na kusema ni kupoteza muda pamoja na fedha kwakua mchezaji mzuri huwa hajaribiwi anasajiliwa moja kwa moja.

"Azam waliwaleta Pascal Wawa na Kipre Tchetche wakasajiliwa moja kwa moja na hadi leo wapo kikosi cha kwanza sasa hao wanaoletwa leo na baada ya wiki wanarudishwa si uharibifu wa hela tu huku wakiwa hawana msaada wowote," alihoji Julio.

Nae kiungo mpya wa klabu hiyo aliyekuwa akicheza Toto Africa Abdala Seseme alisema ana imani kikosi chao kitafanya vizuri zaidi msimu ujao baada ya kuwa na kikosi chenye muunganiko wa vijana na wakongwe.

Post a Comment

 
Top