BOIPLUS SPORTS BLOG

PARIS, Ufaransa

URENO imetawazwa mabingwa wapya wa kombe la Euro 2016 baada ya kuwachapa wenyeji Ufaransa kwa goli 1-0 katika dakika za nyongeza kwenye uwanja wa Stade de France.

Katika fainali hiyo mchezaji bora wa dunia mara tatu Cristiano Ronaldo alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumizwa na kiungo Dimitr Payet dakika ya 20 nafasi ikachukuliwa na Ricardo Quaresma.

Wenyeji walikuwa bora na walimiliki mpira kwa kiasi kikubwa huku kiungo Mousa Sissoko akionesha kandanda safi na kupiga mikwaju mikali langoni mwa Ureno lakini golikipa Rui Patricio alikuwa kikwazo kikubwa.

Kocha wa Ureno Fernando Santos alifanya mabadiliko katika eneo la kiungo kwa kuwatoa Andrien Silva na Renato Sanchez nafasi zikachukuliwa na Joao Moutinho pamoja na Eder hali iliyowarudisha mchezoni.


Dakika ya 109 mshambuliaji Eder alipatia Ureno goli la ushindi kwa shuti kali nje kidogo ya kisanduku cha hatari baada ya kupokea pasi toka Moutinho.

Wenyeji walionekana kulisakama lango la Ureno huku pia suala la bahati likiwa halikuwa upande wao baada ya mipira ya Andre Gignac kugonga nguzo na kuokolewa.

Ubingwa huu unamsafishia njia Ronaldo kupata tuzo ya Ballon d'O baada ya kuisaidia nchi yake kuibuka machampioni na klabu yake Real Madrid kupata ubingwa wa ligi mabingwa barani Ulaya.


Post a Comment

 
Top