BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

LICHA ya kuondokewa na wachezaji nyota wanne wa kikosi cha kwanza, timu ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro imeonyesha kuwa haitatetereka na kwamba watatisha na vipaji vipya msimu ujao.

Wachezaji Shiza Kichuya, Mohammed Ibrahimu na Muzamir Yassini wamejiunga na Simba huku Andrew Vicent 'Dante' akisaini kandarasi na mabingwa wa ligi kuu timu ya Yanga.

Kocha wa wakata miwa hao Salum Mayanga aliiambia BOIPLUS kwenye mazoezi ya timu hiyo yalifanyika kwenye ufukwe wa Coco kuwa kuondoka kwa nyota hao kunatoa nafasi kwa wachezaji wengine kuonesha vipaji vyao na kuziba nafasi hizo.

"Tumeondokewa na wachezaji wetu wanne lakini timu bado ipo vizuri tutaongeza wachezaji wengine pamoja na kupandisha vijana chipukizi," alisema Mayanga aliyemrithi Mecky Maxime.

Aidha Mayanga alisema maandalizi wanayoyafanya kuelekea kufunguliwa kwa pazia la ligi kuu Tanzania bara mwezi ujao ni mazuri huku akihitaji mechi zisizo pungua tano kwa ajili ya kujipima ubavu.

"Tunahitaji mechi zisizo pungua tano kwa ajili ya maandalizi ili kuiandaa timu kimashindano kabla ya kufunguliwa kwa pazia la ligi" alisema Mayanga.

Mtibwa imeweka kambi jijini Dar es Salaam kujiwinda na mikiki ya ligi kabla ya kurejea mkoani Morogoro tayari kwa mapambano.

Post a Comment

 
Top