BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
RAIS wa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) Jamali Malinzi amefungua kozi ya ukocha wa leseni daraja A ya CAF ambayo ndiyo ya juu zaidi barani Afrika.

Kozi hiyo itawashirikisha makocha 20 ambao watakuwa chini ya wakufunzi Salum Madadi na Sunday Kayuni kwa muda wote ili kuwaandaa walimu hao na baadae waje kuwa msaada mkubwa kwa taifa.

Aidha Malinzi alisema imefikia hatua sasa nchi ya Tanzania kutoa makocha wengi kufundisha mpira nje ya nchi ambao wataitangaza nchi katika medani ya soka kote ulimwenguni.

"Tuna idadi ndogo sana ya makocha wenye leseni A ambapo hadi sasa wapo 23 huku wanaofundisha mpira  ni saba pekee, kwahiyo kazi tuliyonayo bado ni kubwa" alisema Malinzi.

Kwa upande wake Mkufunzi wa kozi hiyo Salum Madadi amelipongeza shirikisho la miguu Tanzania kwa kuandaa kozi hiyo inayotambuliwa na CAF ambayo itazalisha makocha wengi wa mpira nchini.

"Nachukua nafasi hii kumpongeza Rais Malinzi kwa kuandaa kozi hii ambayo ni faida kubwa kwa taifa miaka michache ijayo" alisema Madadi.

Wakati huo huo Malinzi ametoa rai kwa makocha hao kuendelea kufundisha soka nchini watakapo hitimu kozi hiyo ili waendeleze ujuzi walioupata kwa vitendo.

Post a Comment

 
Top