BOIPLUS SPORTS BLOG

Karim Boimanda, Dar
'SUBIRA yavuta heri', lakini 'Ngoja ngoja yaumiza tumbo'. Baada wapenzi wa Simba kusubiri ujio wa straika Laudit Mavugo kwa kipindi kirefu, hatimaye hadithi imefika mwisho kuwa nyota huyo hatokuja nchini.

BOIPLUS ilimtafuta Mavugo kutaka kujua anatua lini kwa Wekundu hao ndipo mfumania nyavu huyo alipofunguka kuwa ameshatimkia nchini Ufaransa kufanya majaribio katika klabu ya Tours  inayoshiriki ligi daraja la pili.

"Niliondoka Burundi jana lakini si safari ya kuja huko Tanzania, nimekuja Ufaransa kufanya majaribio kwenye klabu ya Tours," aliongea Mavugo kwa kifupi.

BOIPLUS ilipomtafuta Rais wa Simba, Evans Aveva ili kujua kama timu hiyo iliyo katika mapambano ya kukijenga kikosi chake ina taarifa juu ya Mavugo kutimkia Ufaransa, kiongozi huyo mkuu alisema uongozi wake haujui lolote.

"Hatuna taarifa yoyote, tulitarajia angetua wikiendi hii lakini hapatikani hewani. Hatuelewi kinachoendelea ila tutafuatilia na tutajua cha kufanya," alisema Aveva.

Simba imekuwa ikimfuatilia mshambuliaji huyo tangu mwaka jana na ikafikia hatua ya kumpatia dola 10,000 kama 'kishika uchumba' lakini kumekuwa na hadithi tu juu ya ujio wake na endapo atafuzu katika majaribio hayo basi wekundu hao watalazimika kuweka silaha chini.

Post a Comment

 
Top