BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KOCHA mpya wa Kagera Sugar Mecky Maxime amemaliza suala la usajili ndani timu yake na sasa yupo kwenye maandalizi ya kusuka kikosi kabambe kwa ajili ya msimu mpya utakaoanza Agosti 20.

Maxime ambaye msimu uliopita alikuwa akiwanoa wakata miwa wa Mtibwa Sugar amekuwa miongoni mwa walimu vijana wazawa walioweza kuwapa changamoto makocha wa kigeni hasa wa timu za Simba,Yanga na Azam.

Kocha huyo ameiambia BOIPLUS kuwa ameshapeleka mapendekezo kwa uongozi wa timu kuhusu wachezaji anaowahitaji ndani ya kikosi huku asilimia kubwa yakiwa yamefanyiwa kazi.

"Nilishapeleka ripoti kwa uongozi kuhusu aina ya wachezaji ninaowahitaji kikosini na kwa asilimia kubwa imefanyiwa kazi kitu kinachonipa faraja katika kazi yangu," alisema Mecky.

Aidha kocha huyo alisema angeweza kwenda timu yoyote alipotoka Mtibwa kikubwa ila alichoangalia ni maslahi mazuri na mazingira bora ya kazi.

"Mimi hata ukiniita nyumbani kwako nikufundishie mwanao peke yake nipo tayari ninachoangalia ni maslahi na mazingira mazuri ya kazi," alisema nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa na Taifa Stars.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na shirikisho la mpira wa miguu Tanzani (TFF) Kagera itaanza kampeni ya ligi kuu kwa kuikaribisha Mbeya city katika uwanja wa Kaitaba ambao msimu uliopita ulikuwa katika marekebisho ya uwekaji nyasi bandia.

Mecky amechukua mikoba iliyoachwa na kocha Adolf Rishard aliyefanikiwa kukinusuru kikosi hicho na janga la kushuka daraja.

Post a Comment

 
Top