BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

PAMOJA na kuambulia vipigo viwili mfululizo toka kwa Mo Bejaia na TP Mazembe katika kombe la shirikisho barani Afrika bado wachezaji wa timu ya Yanga wanaamini wana nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali.

Kauli hiyo imetolewa na kiungo mshambuliaji Deus Kaseke na kuwataka wapenzi na wanachama wa klabu hiyo kutokata tamaa na matokeo waliyopata nadala yake waangalie michezo iliyo mbele yao.

Yanga itashuka dimbani kati ya Julai 15 na 17 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kukipiga dhidi ya Madeama City toka Ghana katika mchezo ambao kwa udi na uvumba wanatakiwa kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.

"Bado tunayo nafasi ya kusonga mbele kwakuwa tumecheza mechi mbili na kubakiwa na nne kwahiyo endapo tutashinda michezo yetu yote tutakuwa katika nafasi nzuri," alisema Kaseke.

Aidha Kaseke ameiambia BOIPLUS kuwa wachezaji wote wana ari na morali ya kufanya vizuri katika michezo yao iliyobaki huku wakiwa na imani ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.

"Wachezaji tuna ari kubwa na tuna imani yakufanya vizuri katika mechi zetu zilizobaki, tunawaomba wapenzi wetu wasikatishwe tamaa na matokeo yaliyopita" alisema Kaseke.

Kaseke ni miongoni mwa wachezaji wanaoaminiwa na kocha Hans Pluijm tangu alipojiunga na mabingwa hao msimu uliopita akitokea Mbeya City.

Post a Comment

 
Top