BOIPLUS SPORTS BLOG

PARIS,Ufaransa

MICHUANO ya Euro inayoendelea nchini Ufaransa imefikia hatua ya Fainali ambapo wenyeji watacheza na Ureno ambao hawakupewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri au hata kufika katika hatua hiyo. Mtanange huo utachezeshwa na refa Muingereza Mark Clattenberg katika uwanja wa Stade de France wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 81,338.

Ufaransa wataendelea kumtumia kinara wa ufungaji Antoine Griezmann ambaye tayari amefunga magoli sita huku akiwapa presha kubwa walinzi wa Ureno wakiongozwa na Pepe. Upande wa pili mchezaji bora mara tatu wa dunia Cristiano Ronaldo ana jukumu zito la kuisaidia nchi yake kubeba kombe ili ajiweke katika nafasi nzuri ya kuchukua tuzo ya Ballon d'Or  kwa mara ya nne mwezi Januari mwakani endapo atafanikiwa.

Ufaransa na Ureno zimewahi kukutana mara kadhaa katika michuano mbali mbali na mechi za kirafiki. Zifuatazo ni mechi tano za kukumbukwa zaidi baina ya miamba hiyo ya Ulaya.

5. Ufaransa 5-3 Ureno (11 Novemba 1959)

Hii ilikuwa ni mechi ya kirafiki lakini ilikuwa na mvuto wa aina yake kutokana na kuzalisha magoli mengi na kutoa burudani kubwa kwa watazamaji waliohudhuria.​

Mchezo huo ulichezwa katika uwanja wa  Stade De Colombes jijini  Paris wenye uwezo wa kuingiza watazamaji  48,000,ambapo ni chimbuko la wachezaji wengi wa Ufaransa. 

Katika mchezo huo mshambuliaji Diego Fontine alifunga mabao matatu 'hattrick' na kuwasambaratisha Wareno.

4. Ufaransa 3-2 Ureno(23 Juni 1984)

Michae Platini aliifungia Ufaransa goli la kwanza dakika ya 19 lakini baadae Jordao alisawazisha na kuongeza la pili na kuwaacha Les Blues midomo wazi.​

Wafaransa waliongeza kasi kabla ya Jean-Francois Domergue kusawazisha na Platini tena kufunga goli la ushindi.

3. Ufarans 3-2 Ureno (24Januari1996)

Mechi nyingine baina ya mataifa hayo ilikuwa ni ya kirafiki baada miaka 12. Ufaransa waliendelea kuwanyanyasa Ureno mchezo ambao uliyakutanisha mataifa hayo tangu michuano ya Euro ya mwaka​1984.

Ureno ilipata magoli mawili ndani ya dakika 31 kupitia kwa Fernando Couto na Rui Costa kabla ya Oliver Djorkaeff kufunga magoli yote matatu na kuendeleza ubabe wa kila mchezo wanaokutana.

2. Ufaransa 2-1 Ureno (28 Juni 2000)

Huu ulikuwa mchezo wa nusu fainali ambao Ufaransa walikuwa katika ubora wa hali juu wa kusakata kabumbu. Ulikuwa ni usiku ambao Zinedine Zidane alicheza  soka safi na ndiye aliyekuwa akiamua matokeo ya mchezo huo. Abel Xavier aliunawa mpira wa krosi wa Sylain Wiltord na Zidane akafunga penalti hiyo kwa ustadi mkubwa na baadae Thiery Henry alifunga goli la ushindi.

1. Ufaransa 1-0 Ureno (5 Julai 2006)

Hii ilikuwa ni katika michezo ya fainali ya kombe la dunia ​iliyofanyika nchini Ujerumani. Mtanange huo ulikuwa mgumu sana kwa upande wa Ufaransa kutokana na ubora wa kikosi cha Ureno lakini siku hiyo hawakuwa na bahati.

Ureno walitengeneza nafasi nyingi lakini Cristiano Ronaldo, Luis Figo and Fernando Meira walimshindwa kuzitumia kabla vijana wa kocha Raymond Domanech kuja juu na kupata ushindi wa goli 1-0.

Kwa mujibu wa matokeo ya michezo  mitano waliyokutana miamba hiyo ya soka barani Ulaya Ufaransa inapewa nafasi kubwa ya kubakisha kombe katika ardhi ya nyumbani lakini mpira siku zote unadunda na unakuwa na matokeo ya ajabu sana wakati mwengine.


Imeandaliwa na Bakari Kagoma kwa msaada wa mitandao.

Post a Comment

 
Top