BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu

BAADA ya kuwatoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa , timu ya soka ya Vijana wenye umri  chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imebakiza mitihani miwili kabla ya kuandika historia ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, imefahamika.

Mtihani wa kwanza ni mchezo dhidi ya Afrika Kusini unaotarajiwa kufanyika kati ya Agosti 5, 6 au 7 ambako mechi ya kwanza itapigwa ugenini kabla ya kurudiana jijini Dar es Salaam wiki moja baadae  mchezo utafanyika Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamazi Agosti 14.

Mshindi wa jumla katika michezo hiyo, atacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville. Wakati Afrika Kusini imepitishwa moja kwa moja Namibia imepenya kwa kuiondoa Botswana licha ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wake uliofanyika jana Julai 2,  huko Botswana.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime, ameangalia ratiba hiyo na kusema “Ushindani utakuwa mkubwa, lakini mimi nimelenga kushinda michezo yote iliyo mbele yangu. Si kwamba napigania kufuzu kwenda Madagascar tu kwenye fainali za Afrika, la hasha, nataka timu hii niipeleke Kombe la Dunia.”

Fainali za Kombe la Dunia, mwakani zitapigwa nchini India ambako kama Serengeti Boys itafuzu kucheza fainali za Afrika na ikaingia nusu fainali kwa maana timu nne bora zote zitashiriki fainali hizo ambazo tayari Tanzania imejiwekea mazingira mazuri ya kufuzu.

“Timu hii nimeanza nayo zaidi ya mwaka mmoja. Sioni kama itakuwa kikwazo kuifanikisha kufika fainali za Kombe la Dunia. Namuomba Mungu atunyooshee mkono wake, nawaombea viongozi wa TFF wazidi kuihudumia timu hii, lakini pia wadau wengine waisapoti timu hii bila kuangalia au kuchagua mtu anayeongoza TFF. Hii ni timu ya Watanzania wote,” amesema Shime maarufu kama Mchawi Mweusi.

Shime alishukuru mipango na ahadi ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi kugharamia kambi ya wiki mbili itakayofanyika Madagascar kuanzia Julai 24, mwaka huu akisema: “Hii itakuwa ni kambi bora. Kwa sasa kikosi changu kinahitaji utulivu hivyo kwa maoni na mipango yangu naona inafaa.”

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu kwa Vijana anayeongoza timu hiyo, Ayoub Nyenzi kadhalika aliomba sapoti ya Watanzania ili kuendeleza timu hiyo, amesema: “Hakika nikipata watu wakutuunga mkono, naamini ndoto zetu zitatimia .”

Nyenzi amethibitisha kwamba timu hiyo itaondoka hapa jijini Victoria kesho Jumatatu Julai 4, saa 11.00 jioni   na inatarajiwa kufika Tanzania saa 7.45 usiku wa kuamkia Jumanne Julai 5.

“Wachezaji watakuwa na mapumziko mafupi kabla ya kuanza kambi ya maandalizi kwenda Madagascar kwenye kambi ya kuiandaa timu kucheza na Afrika Kusini,” alisema Nyenzi.

Post a Comment

 
Top