BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

LICHA ya kusajiliwa viungo bora na klabu ya Simba msimu ujao nahodha msaidizi wa timu hiyo Jonas Mkude hatishiki na ujio wao na amewakaribisha kiroho safi.

Simba tayari imewasainisha viungo Mohammed Ibrahim pamoja na Muzamiru Yassin toka Mtibwa Sugar ambao walicheza katika kiwango bora msimu uliopita wakiwa na Wakata miwa hao kiasi cha kutishia namba kwa wachezaji waliokuwepo kwenye kikosi cha kwanza cha Wekundu hao.

Akizungumza na BOIPLUS Mkude alisema ahofii Simba kusajili viungo wazuri na kwba anachozingatia ni kufanya mazoezi kwa kujituma nakufuata maelekezo ya mwalimu ambaye ndiye mwamuzi wa mwisho kuhusu nani aanze katika mechi ipi.

"Ni wachezaji wazuri,tumekutana mara nyingi kwenye mechi za ligi ila hawanipi presha, ninajiamini niko fiti kuitumikia na kuisaidia Simba msimu ujao tuweze kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita," alisema Mkude.

Mkude pia amefurahishwa na mwenendo wa usajili unaofanywa na uongozi wa klabu yake huku akitanabaisha kuwa endapo majina ya wachezaji wanaotajwa kujiunga na Simba watasajiliwa watakuwa na msaada kwa Wekundu hao msimu ujao.

Kiungo huyo anayeamini ushindani wa namba kikosini ndio unaoifanya timu iwe nzuri alimzungumzia pia kocha wao mpya Joseph Omog kuwa ni mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchezaji ndani ya Simba kutokana na soka analofundisha.

Omog ndiye kocha wa kwanza kuipa ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara klabu ya Azam FC mwaka 2014.

Post a Comment

 
Top